1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa washirika Stuttgart kupambana na IS

Admin.WagnerD4 Mei 2016

Mataifa 11 washirika wa muungano unaoongozwa na Marekani katika mapambano dhidi ya kundi la IS nchini Iraq na Syria, yanafanya mkutano wao mjini Stuttgart leo kuweka mikakati juu ya kuongeza usaidizi kwa Iraq.

https://p.dw.com/p/1IhYp
USA Verteidigungsminister Ashton Carter
Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton CarterPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Martinez Monsivais

Mikakati hiyo ni juhudi za kuisaidia Iraq kuukamata tena mji wa Mosul ambao ni ngome kuu ya kundi hilo la IS.

Kikao hicho ni cha hivi karibuni kabisa katika mlolongo wa mikutano kama hiyo ya washirika kuweka mikakati ya kuongeza usaidizi kwa Iraq ili kuikamata ngome ya kundi la IS upande wa kaskazini mwa Iraq ya Mosul.

Irak Militär Operation gegen IS
Mapambano nchini IraqPicha: Getty Images/AFP/M. Al-Dulaimi

Hii inakuja wakati mzozo wa kisiasa katika serikali ya mjini Baghdad unaweka kiwingu katika muonekano wa mafanikio zaidi ya kijeshi dhidi ya wanagambo wa Dola la Kiislamu.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter amesema wakati akiwasili mjini Stuttgart kuhudhuria mkutano huo kwamba kifo cha mwanajeshi wa Marekani katika mapambano nchini Iraq kinaonesha kwamba kampeni ya kijeshi dhidi ya kundi la Dola la kiislamu , "bado hayajaisha."

Marekani yawataka washirika kuweka nguvu zaidi

Carter ameweka umuhimu wa juu katika kuwavuta washirika ndani zaidi ya kampeni ya kupambana na IS, akisisitiza kitisho kilichopo kwa kuwaruhusu wanamgambo hao wenye itikadi kali kusambaza ushawishi wao.

Kämpfe in Ramadi
Mapambano katika mji wa Ramadi nchini IraqPicha: picture-alliance/AP Photo

kundi la Dola la Kiislamu lilimuua mwanajeshi wa Marekani kaskazini mwa Iraq jana Jumanne baada ya kupiga katika ngome za ulinzi za wapiganaji wa Kikurdi na kuukamata mji mmoja katika shambulio kubwa katika eneo hilo kwa muda wa miezi kadhaa, wamesema maafisa.

Mwanajeshi huyo anakuwa wa tatu kutoka marekani kuuwawa katika mapambano ya moja kwa moja tangu muungano unaoongozwa na Marekani kuanzisha kampeni hiyo mwaka 2014 "kuharibu ili kuvuruga uwezo" wa kundi la Dola la Kiislamu na ni hatua ya kuingia zaidi katika mzozo huo.

"Ni kweli kwamba ni kifo katika mapambano , na ni kifo kinachosikitisha," amesema waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton carter wakati alipokuwa akizungumza na waandishi habari wakati wa ziara nchini Ujerumani.

Navy Seal Rob O'Neill
wanajeshi wa kikosi cha Navy SEAL cha MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Kikosi cha SEAL

Afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani , akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina , amesema mwanajeshi huyo aliyeuwawa alikuwa katika kikosi maalum cha SEAL.

Wanajeshi wa kikosi hicho wanaonekana kuwa miongoni mwa wanajeshi maalum wa Marekani wenye uwezo mkubwa na wanaoweza kuingia katika maeneo hatari. Jina na cheo cha mwanajeshi huyo havikutajwa na wizara ya ulinzi ya Marekani.

Gavana wa jimbo la Marekani la Arizona , Doug Ducey , alimtaja mwanajeshi huyo aliyeuwawa kuwa ni Charlie Keating IV, na kusema Keating alihudhuria masomo yake ya juu katika shule mjini Phoenix.

Navy Seals ARCHIVBILD 2007
Mwanajeshi wa kikosi maalum cha Navy SEALPicha: Getty Images

Gazeti la San Diego Union-Tribune , la califonia kusini, limemweleza mwanajeshi huyo ambaye hakutajwa na ndugu zake katika taarifa yake kuwa Keating alikuwa ni mjukuu wa Charles Keating Jr.,mfanyakazi wa benki ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kashfa ya masuala ya kuweka akiba na mikopo nchini Marekani ya miaka ya 1980 ambayo iliwahusisha maseneta watano wa Marekani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape

Mhariri: Yusuf Saumu