Mkutano wa waislamu Berlin
2 Mei 2007Mkutano wa pili wa Jumuiya ya waislamu nchini Ujerumani, unafunguliwa hii leo mjini Berlin.Mkutano wa kwanza uliitishwa Septemba mwaka jana na waziri wa ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble.
Katika kikao hiki cha pili, inapangwa kuzingatia matokeo yaliofikiwa na halmashauri mbali mbali zilizopewa jukumu maalumu.
Shabaha ya siku za usoni kabisa ya mkutano huu wa waislamu nchini Ujerumani ni kuwaunganisha pamoja waislamu kiasi cha milioni 3.5 na jamii ya wajerumani badala ya kama ilivyokua hadi sasa kuwa pembezoni na kutokua na msemaji au jumuiya ya kuwakilisha masillahi ya waislamu humu nchini.
Kabla kuanza kikao cha hii leo, ziliibuka tofauti wazi kati ya jumuiya m,bali mbali za waislamu waishio humu nchini na serikali ya Ujerumani.
Waziri wa ndani wa Ujerumani Bw.Schauble,hakuzipa jumuiya hizo kuwasemea waislamu wote wanaoishi humu nchini.Baraza la waislamu-Islamrat na Baraza kuu la waislamu-Zentralrat-yamemkosoa waziri wa ndani Bw.Schauble kwa matamshi hayo.Waziri huyo anaona lakini, licha ya mabishano yaliopo kati yao kuna maendeleo yaliofanyika katika juhudi za kuwajumuisha waislamu wanaoishi humu nchini na jamii.
Katika ukumbi wa chuo cha taftishi cha Berlin-Brandenburg, wanahudhuria leo wajumbe 13 kutoka upande wa serikali ya ujerumani na wajumbe 5 wa jumuiya muhimu za kiislamu za humu nchini.
Mkutanoni pia wanawakilishwa wajumbe 9 wa kiislamu wasio wanachama wa jumuiya au baraza lolote la kiislamu na miongoni mwao kuna wakosoaji.
Waziri wa ndani wa Ujerumani ametangaza kuundwa kwa halmashauri zitakazokuwa na jukumu la kupanga mikakati ambayo itapelekea kutambuliwa kwa uislamu kama ni jumuiya ya kidini humu nchini hadhi ambayo bado haikupatiwa waislamu.
Msemaji wa baraza la maandalio ya mkutano wa leo Ayub Axel Köhler,ameueleza mkutano huu kuwa ni utaratibu wa kujuana na kutafutana.Njia ya kufikia shabaha za mkutano huu wa waislamu zitapaswa lakini, anasema ,kufafanuliwa barabara.
Hata Bw.Köhler anatetea dini ya kiislamu nchini Ujerumani kuwekwa safu sawa na dini nyenginezo nchini humu.Wakati huo huo akapendekeza kuwapo mpango maalumu-au kile alichokiita “Road map”-ramani ya kufuatwa kufikia shabaha hiyo.
Waziri wa mkoa wa Northrhine-westphalia anaehusika na kuwajumuisha wageni na jamii ,Armin Laschet,amelieleza Baraza hili la mipango la waislamu kuwa chombo muhimu kufikia lengo la kuwa na jumuiya ya kidini.
Akalitetea baraza hilo na tuhuma kwamba, linawakilisha waislamu wahafidhina.Hawa ni waislamu wanaokwenda kila siku kuabudu misikitini na kujisghulisha na dini yao.Yamkini, anaungama ni waislamu wahafidhina.Aliwataka lakini, wale waislamu wasio-wahafidhina nao kujiandaa katika jumuiya zao.
Mjumbe wa chama cha upinzani cha walinzi wa mazingira-KIJANI- Volker Beck, alionya mkutano huu wa leo wa waislamu, usigeuzwe jukwaa la porojo tupu.