1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa umoja wa Afrika waanza mjini Addis Ababa.

Sekione Kitojo2 Februari 2009

Mkutano wa umoja wa Afrika umeanza rasmi jana Jumapili mjini Addis Ababa , ukiangalia kwa undani suala la kujenga mifumo ya usafirishaji na nishati, pamoja na mizozo katika bara hilo.

https://p.dw.com/p/GlWS
Kiongozi wa Libya Muammar el Gaddafi. ambaye aliongoza miito ya kutaka kuundwa serikali ya muungano wa Afrika katika siku ya kwanza ya mkutano wa viongozi wa umoja wa Afrika mjini Addis Ababa wiki hii.Picha: dpa/picture-alliance


Mkutano wa Umoja wa Afrika umeanza rasmi jana Jumapili mjini Addis Ababa, ukiangalia kwa undani suala la kujenga mifumo ya usafirishaji na nishati, lakini pia mkutano huo umegubikwa na matatizo ya mizozo katika bara hilo na mgawanyiko kuhusu hali ya baadaye ya umoja huo.

Ni viongozi 20 tu kutoka nchi wanachama 53 ambao wamehudhuria siku ya mwanzo ya kikao hicho, kilichofanyika kwa faragha na kujadili juu ya iwapo Umoja wa Afrika unaweza kubadilika na kuwa katika mfumo wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya utawala wa eneo hilo.

Kiongozi wa Libya Moammar Ghadafi aliongoza miito ya umoja wa Afrika kuunda serikali ya muungano ambayo anaamini itaimarisha heshima ya Afrika kimataifa, lakini alishindwa kupata wingi wa waungaji mkono wa hoja yake miongoni mwa viongozi wenzake ambao hawakutaka kupoteza madaraka yao na utaifa.

Katika muafaka, mkutano huo umekubaliana kuibadilisha halmashauri ya umoja wa Afrika , ambayo kwa hivi sasa inaongoza umoja huo, kuwa mamlaka ya umoja wa Afrika ambayo itakuwa na mamlaka makubwa, rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amewaambia waandishi wa habari.

Kimsingi, tumesema lengo ni kuwa na serikali ya muungano wa mataifa ya Afrika. Kikwete ameongeza kuwa , ni vipi tunafikia katika lengo hilo, bado kuna vikwazo.

Tunaunda taasisi itakayokuwa na mamlaka makubwa, yenye uwezo mkubwa, ambayo itatuongoza kuelekea katika lengo la kuwa na serikali ya muungano, ameongeza Kikwete, licha ya kuwa vipengee vya mabadiliko bado vinajadiliwa.

Wakati ajenda kuu inamulika kuhusu hali ya baadaye ya umoja huo, mazungumzo yamegubikwa na ghasia na vita nchini Somalia na Madagascar, na kutengwa kwa mataifa ya Guinea na Mauritania kutokana na mapinduzi katika nchi hizo.

Miongoni mwa viongozi wanaoonekana zaidi waliopo katika mkutano huo ni Sheikh Sharif Ahmed , ambaye alichaguliwa kuwa rais mpya wa Somalia siku ya Ijumaa.

Katika hotuba yake ya uzinduzi nchini Djibouti , Sheikh Sharif ameahidi kujenga serikali itakayojumuisha makundi yote, na kuyanyooshea mkono makundi yenye msimamo mkali yenye silaha ambayo bado yanapinga kuwapo mazungumzo ya amani na kuiweka Somalia katika sehemu inayostahili katika jumuiya ya mataifa ya Afrika.

Umoja wa Afrika , ambao una wanajeshi 3,500 wa kulinda amani nchini Somalia, imekuwa ikiyaomba mataifa wanachama na jumuiya ya kimataifa kutoa msaada unaohitajika kupanua ujumbe huo wa kulinda amani hadi katika kiwango chake kilichopangwa cha wanajeshi 8,000.

Mizozo mingine pia imehitaji kuangaliwa na mkutano huo. Wakati mzozo wa kisiasa nchini Madagascar unazidi kuongezeka kila kukicha , mwenyekiti wa halmashauri ya umoja wa Afrika Jean Ping ameonya katika mkesha wa mkutano huo kuwa mabadiliko yoyote ya madaraka ambayo hayatafuata katiba yatashutumiwa.

Sekione Kitojo/AFPE