Mkutano wa Asia a na Ulaya.
23 Oktoba 2008Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewasili mjini Beijing kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya na wa bara la Asia wa jumuiya ya Asem ambapo pande mbili hizo zinatarajiwa kujadili mgogoro wa fedha unaoikabili dunia.
Lakini vyama vya upinzani nchini Ujerumani vinamtaka kansela Merkel pia ajadili suala la haki za binadamu na viongozi wa China.
Kansela Merkel anaefanya ziara ya siku tatu nchini China atakuwa miongoni mwa viongozi 43 kutoka Ulaya na nchi za jumuiya ya Asem watakaokutana kwa siku mbili katika mji mkuu wa China-Beijing kujadili mgogoro wa fedha ambao pia unahitaji juhudi za nchi zinazoinukia kiuchumi katika kuukabili.Kansela Merkel amesema bila ya nchi hizo kushiriki, itakuwa vigumu kusonga mbele na shughuli za masoko ya fedha duniani.
Hatahivyo kiongozi huyo wa Ujerumani anakabiliwa na shinikizo katika ziara yake nchini China.Mwezi septemba mwaka jana alikutana na kiongozi wa kidini wa Tibet anaeongoza upinzani dhidi ya China.
China inapinga mikutano baina ya kiongozi huyo Da Lai Lama na viongozi wa nchi zingine.
Wakati huo huo vyama vya upinzani nchini Ujerumani vinamtaka kansela Merkel ajadili suala la haki za binadamu.
Kiongozi wa wabunge wa chama cha kijani Volker Beck amesema bibi Merkel anapaswa kuwasilisha msimamo wa Ujerumani kwenye mikutano yake na viongozi wa China juu ya suala la haki za binadamu na hasa kuhusiana na hali ya majimbo ya mashariki mwa China.
Wakati huo huo waziri mkuu wa China Wen Jiabao amesema nchi yake inadhamiria kushirikiana kwa undani sana, na Ujerumani ili kukabili nyakati ngumu za sasa. Waziri mkuu Jiabao amesema hayo kwenye mazungumzo yake na Kansela Merkel. Amesema China inakusudia kushirikiana na Ujerumani katika juhudi za kujenga mfumo mpya wa fedha duniani.
Hapo kesho Kansela Merkel ataungana na viongozi wengine 42 kushiriki kwenye mkutano wa saba wa kilele baina ya marais na mawaziri wakuu nchi za Ulaya na za jumuiya ya Asem. Kikao hicho cha siku mbili kitatayarisha mkutano wa viongozi kutoka nchi 20 utakaofanyika kati kati ya mwezi Novemba kujadili mfumo wa fedha wa dunia. Ujerumani na China pia zitashiriki kwenye mkutano huo mjini Washington.