1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa Korea waendelea

Sekione Kitojo3 Oktoba 2007

Akisingiziwa maovu, akikejeliwa na hisia za hofu kutoka mataifa ya nje, kiongozi wa Korea ya kaskazini mwenye usiri Kim Jong – Il amekuwa akipambwa kwa sifa za mara kwa mara nchini mwake kuwa ni mtu mwenye busaza zinazokaribia za uungu pamoja na vipaji.

https://p.dw.com/p/CH7G
Kiongozi wa Korea Kusini kwa mara ya kwanza alivuka mpaka
Kiongozi wa Korea Kusini kwa mara ya kwanza alivuka mpakaPicha: AP

Siku ya Jumatano Kim mwenye umri wa miaka 65 alikuwa mwenyeji wa mkutano wa pili baina ya Korea mbili. Mkutano huo na kiongozi wa Korea ya kusini Roh Moo-hyun unafanyika ikiwa ni makubaliano ya kihistoria pamoja na mataifa makubwa ya eneo hilo ambayo yanaonekana kufikisha tamati nia ya Korea ya kaskazini kusaka silaha za kinuklia.

Akielezewa kuwa ni kiongozi mpenzi na vyombo vya habari nchini mwake ambavyo anavithibiti, Kim alirithi moja kati ya mataifa yaliyo na usiri mkubwa duniani mwaka 1994 baada ya kifo cha baba yake, mwasisi wa taifa hilo Kim Il-sung, akiunda ukoo wa kwanza wa kikomunist.

Anatambulika rasmi kuwa alizaliwa katika kambi ya siri ya wapiganaji wa chini kwa chini dhidi ya Japan karibu na Peaktu-san eneo lililoko milimani katika mpaka na China mahali ambapo hivi sasa panaangaliwa kama sehemu ya hija. Wadadisi wa mambo wanasema kuwa inawezekana pia kuwa sehemu alikozaliwa ni nchini Urusi ambako baba yake alikuwa akipata mafunzo pamoja na Wakorea waliokuwa wakiishi uhamishoni.

Tangu pale alipoingia madarakani , ameweza kwa kiasi kikubwa kujenga nafasi ambayo hakuna mtu anayeweza kumpinga kwa madaraka licha ya kuliongoza taifa hilo la kikomunist akiliona linatumbukia katika umasikini, njaa katika miaka ya 90 na utegemezi mkubwa wa misaada kutoka nje katika nchi hiyo ambayo nadharia ya taifa ni kujitegemea.

Lakini kwa upande wa mataifa ya kigeni, kiongozi huyo , ambaye amekuwa lengo la kejeli anashutumiwa kwa kukandamiza haki za binadamu na kuleta kitisho duniani na nia yake ya kujipatia silaha za kinuklia. Katika miaka ya 1980 , kabla ya kuwa kiongozi wa nchi hiyo, anaaminika kuwa alipanga mauaji ya maafisa 17 wa ngazi ya juu wa Korea ya kusini wakiwa ziarani nchini Myanmar, wakati huo ikiitwa Burma , pamoja na shambulio la ndege ya abiria ikiwa angani ya shirika la ndege la Korea ambapo watu 115 waliuwawa.

Ziara aliyoifanya kwa ajili ya mkutano wa kwanza baina ya Korea mbili katika historia ya miongo sita ya kugawika kwa nchi hizo mbili zilizoko katika rasi, huenda ilikuwa ni nafasi yake muhimu sana Kim Jong-Il katika medani ya kimataifa. Kulikuwa wakati huo na uhusiano lakini uliodumu kwa muda mfupi na mataifa ya magharibi , ambapo haraka ulitoweka baada ya kuingia George W. Bush madarakani katika Ikulu ya Marekani mapema 2001 na kuiingiza nchi hiyo katika kile alichokieleza kama mhimili wa uovu.

Mwaka uliofuata, mahusiano yaliongezeka kuwa mabaya zaidi wakati Marekani ilipoishutumu Korea ya kaskazini kwa kukiuka makubaliano ya hapo awali ya kusitisha shughuli za kutengeneza silaha za kinuklia. Kim Jong Il anaripotiwa kuwaambia watu waliomtembelea kuwa anataka kutimiza wasia wa baba yake kabla ya kufariki kuwa anataka kuliona eneo la rasi ya Korea ikiwa haina silaha za kinuklia, lakini kwanza anataka kuiona Marekani ikiipa heshima nchi yake.