Mkutano wa viongozi wa G8 waingia siku yake ya pili huko L'Aquila, Italia
9 Julai 2009Viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani G8 wanaendelea na mkutano wao huko L'Aquila, Italia, ambapo leo wanajadiliana kuhusu hoja itakayokubaliwa kwa pamoja juu ya ongezeko la ujoto duniani na biashara ya kimataifa, huku nchi masikini zikiwa zinatafuta nafuu.
Rais Baracka Obama wa Marekani ataongoza majadiliano ya hali ya hewa, lakini akiwa na matumaini ya kukubaliana juu ya malengo yaliyofifia baada ya nchi za China na India kukataa kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira ifikapo mwaka 2050.
Mazungumzo hayo ya leo yanafanyika katika siku ya pili ya mkutano huo wa siku tatu wa nchi za G8, ambapo katika siku ya kwanza hapo jana viongozi hao walijadiliana kuhusu uchumi wa dunia, ambapo nchi hizo za Marekani, Japan, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Canada na Russia zikikiri kuwa bado kuna mashaka katika kuimarisha uchumi duniani.
Viongozi hao pia walijadiliana kujaribu kudhibiti ongezelo la ujoto duniani kwa nyuzi selisiasi 2, na kuahidi kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira kwa kati ya asilimia 50 na 80, ifikapo katikati ya karne hii. Akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kwa majadiliano ya leo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amesema ana matumaini kuwa nchi zote zinazoshiriki mkutano huo zitakubaliana kuhusu lengo hilo.
Mkutano huo unaohudhuriwa na nchi za G8 na nchi zinazoinukia kiuchumi leo zinatarajia kukubaliana kuhusu kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira, lakini utekelezaji kamili wa makubalino hayo utafikiwa katika kikao kijacho cha Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa hapo mwezi Desemba, mwaka huu, mjini Copenhagen, nchini Denmark.
Hata hivyo, maendeleo ya majadiliano hayo yanaweza kukwama kufuatia kutokuwepo kwa Rais Hu Jintao wa China aliyerejea nchini kwake kutokana na mapigano katika mji wa Xinjiang uliopo kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu 156 na wengine maelfu kujeruhiwa.
Agenda nyingine itakayotawala katika mkutano wa leo ni kuhusu hali ya uchumi, huku nchi zinazoinukia kiuchumi zikidai kuwa zinaathirika vibaya kutokana na msukosuko wa kiuchumi ambao haukusababishwa na wao.
Aidha, China, India na Brazil zimehoji endapo dunia ianze kutafuta sarafu mpya ya dunia itakayokuwa mbadala wa sarafu ya dola. Wamesema suala hilo huenda wakalizusha katika mkutano wa leo, baada ya kujadiliana miongoni mwao wenyewe hapo jana.
Wanadiplomasia wamesema kuwa nchi za kundi la G8 na zinazoinukia kiuchumi zinatakiwa kukubaliana juu la hitimisho la mazungumzo ya biashara ya mwaka 2010 yaliyokwama yatakayofanyika Doha. Mazungumzo hayo yalianzishwa mwaka 2001 kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini kufanikiwa, yamekuwa yakiyumbayumba kuhusu pendekezo la ushuru wa forodha na kupunguzwa ruzuku.
Nchi zinazoinukia kiuchumi zimezitaka nchi tajiri duniani kuondoa vikwazo vya biashara na kurejesha mikopo kwa nchi masikini. Mkutano huo wa siku tatu utahitimishwa kesho.
Mwansihi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)
Mhariri: Othman Miraji