Mkutano wa viongozi wa Francophonie wamalizika Erewan
12 Oktoba 2018Bibi Louise Mushikiwabo amechaguliwa kwa ridhaa kuwa katibu mkuu wa jumuia ya Francophonie wakati wa kikao cha siri mnamo siku ya mwisho ya mkutano huo wa kilele mjini Erevan nchini Armenia.
Kuchaguliwa bibi Mushikiwabo ni jambo lililokuwa likitarajiwa tangu pale katibu mkuu anaemaliza wadhifa wake, Michaelle Jean, raia wa Canada mwenye asili ya Haiti aliposhindwa kupata uungaji mkono wa nchi yake Canada na pia jimbo la nchi hiyo lenye wakaazi wengi wanaozungumza kifaransa Quebec. Wafadhili hao wawili muhimu wa jumuia ya Francophonie wamelazimika kubadilisha msimamo wao baada ya nchi nyingi zaidi kuamua kuiunga mkono Rwanda.
Kwanza Ufaransa, mfadhili mkubwa wa jumuia hiyo na ambako ndiko rais wa Rwanda Paul Kagame alikotangaza azma ya bibi Mushikiwabo, katika mkutano na waandishi habari pamoja na rais mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron. Wengi wanahisi tangazo hilo ni mpango wa viongozi wa mjini Paris.
Rwanda yakosolewa haiheshimu haki za binaadam
Juhudi za kidiplomasia zimeibuka na ushindi dhidi ya lawama kali zilizofuatia kuteuliwa Rwanda igombee wadhifa wa katibu mkuu wa Francophonie. Lawama hizo ni pamoja na madai kwamba Rwanda haiheshimu haki za binaadamu. Rais Paul Kagame anaeendelea na mhula wa tatu madarakani baada ya kushinda uchaguzi wa rais kwa asili mia 98, ameifanyia marekebisho katiba ili asalie madarakani hadi mwaka 2034. Kwa upande wa lugha, Rwanda iliamua kubadilisha kifaransa kwa kiengereza mwaka 2008 kama lugha ya lazima shuleni kabla ya kujiunga na jumuia ya madola Commmonwealth.
Kumpendekeza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda aongoze jumuia ya Francophonie si ujumbe wa busara kwa wanaozungumza kifaransa ulimwenguni" amelalamika waziri wa zamani wa Ufaransa wa ushirikiano na Francophonie Pierre-André Wiltzer na kusisitiza tunanukuu" "Rwanda iko mbali na kuwa na utawala unaoheshimu uhuru wa kila raia na wa kisiasa katika wakati ambapo mada hizo ndio kitovu cha mwongozo wa jumuia ya Francophonie .
Wanyarwanda wanafurahikia mfumo wao wa kidemokrasi anasema bibi Mushikiwabo
Akihojiwa hivi karibuni na shirika la habari la Ufarasa AFP, bibi Mushikiwabo alikosoa kile alichokiita" "maneno Rwanda inayosingiziwa" akisema wanyarwanda wengi wanapendezewa na mfumo uliopo wa kidemokrasia.
Kwa kuchaguliwa katibu mkuu mpya wa jumuia ya Francophonie Ufaransa inataraji pataibuka muamko ndani ya jumuia hiyo inayolaumiwa kwa kuwa mbali mno na vijana wa kiafrika-lenmgo muhimu la jumuia hiyo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri:Mohamed Abdul Rahman