Wafadhili na wapokea misaada wakutana mjini Accra.
3 Septemba 2008
Wajumbe zaidi ya alfu moja kutoka nchi
wafadhili na zinazoendelea
wanaendelea na mkutano wao mjini
Accra- Ghana, kujadili njia za
kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.
Wajumbe hao wanajadili njia za kuimarisha ushirikiano sambamba na kuhakikisha uwajibikaji katika matumizi ya misaada ya maendeleo. Wapinzani wanasema misaada inayotolewa ni midogo na haina ufanisi. kama anavyoeleza Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali nchini Kamerun Kuenzob anaehudhuria mkutano huo amesema kuwa katika kazi zake za kila siku anashuhudia mashindano baina ya wafadhili wa kimataifa.
Malalamiko kama hayo yametolewa na wajumbe kutoka Kenya,Afghanistan ,Pakistan na kutoka nchi nyingi zinazopokea misaada ya maendeleo.
Njia ya kutatua tatizo hilo ni kuoanisha juhudi za watoaji na wapokeaji misaada, ameeleza Ingrid Gabriela Hoven kutoka wizara ya ushirikiano wa uchumi nchini Ujerumani. Kuhusu urudufu wa miradi, mjumbe huyo kutoka Ujerumani amesema pana haja ya kuzileta pamoja juhudi za wafadhili wa kimataifa ili kuweza kuziratibisha.
Wajumbe kutoka nchi zinazoendelea kwenye mkutano huo wa siku nne mjini Accra nao wamesisitiza umuhimu wa kuzijumuisha asasi za raia katika miradi ya maendeleo. Watetezi wa hoja hiyo wanasema kuwa asasi hizo ndizo zinazoleta maendeleo na siyo serikali.