1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Usalama na hatima ya SPD Magazetini

Oumilkheir Hamidou
19 Februari 2018

Mkutano wa usalama mjini Munich, kisa cha kuachiliwa huru ripota wa gazeti la die Welt nchini Uturuki na jinsi SPD wanavyo tapa tapa kujinusuru wasitoweke katika medani ya kisiasa ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2suiG
54. Münchner Sicherheitskonferenz
Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Tunaanzia mjini Munich, kusini mwa Ujerumani ambako mkutano wa 54 wa kimataifa kuhusu usalama umemalizika jana. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linamulika umuhimu wa kuitishwa mkutano wa usalama katika wakati ambapo hali inatisha ulimwenguni. Gazeti linaendelea kuandika: "Katika wakati ambapo hali ya mambo haikadiriki, ni muhimu kuliko wakati wowote mwengine kwa viongozi wa taifa, wanadiplomasia, na wanasayansi kutoka kila pembe ya dunia kukutana na kubadilishana mawazo. Katika enzi za vita baridi, mikutano kati ya viongozi ndiyo iliyokuwa chanzo cha kuepukwa balaa la vita vya nuklea. Mikutano kama hiyo, inazidi kuwa nadra kuitishwa  siku hizi, naiwe kati ya warusi na wamarekani na katika daraja ya Ulaya, kati ya washirika wa mashariki na wenzao wa magharibi. Hali ya kutojadailiana ndio kitisho halisi kilichoko. Mazungumzo muhimu ya kisiasa mara nyingi hufanyika kwa siri. Mkutano wa usalama umechanagia hali hiyo.  Katika enzi za misuko suko hasa ndipo hatua kama hizo zinapostahiki zaidi kuthaminiwa."

Eti Yücel kaachiliwa huru bila ya maridhiano

Mwandishi habari wa gazeti la die Welt, Deniz Yücel ameachiwa huru kwa ghafla ijumaa iliyopita, baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja jela nchini Uturuki. Eti eti zinahanikiza pengine kuna maridhiano ya aina fulani ya kichini chini yaliyofikiwa kati ya Ujerumani na Uturuki. Serikali kuu ya Ujerumani imekanusha dhana hizo. Gazeti la "Volksstimme" linaandika: "Dalili zinazidi kuongezeka kwamba Deniz Yücel hakutolewa bure jela. Pengine makubaliano ya biashara ya vifaru vya kijeshi, au pengine makubaliano ya kibiashara kwa siku za mbele ndio Erdogan anayoyategemea. Matarajio hayo yatakamilika kwa ziara itakayofanywa si muda mrefu kutoka sasa na maafisa wa ngazi ya juu. Hayo ndio matarajio. Na Erdogan hachelei chochote akipania kutekeleza akitakacho. Anawaonya washirika wake wa NATO atamtia ndani yoyote yule anaemkosoa. Serikali kuu ya Ujerumani isikubali kudanganywa, inabidi iendelee kufuata msimamo mkali. Na sasa kuliko wakati wowote mwengine, Berlin inabidi ishinikize zaidi  mpaka waandishi habari wengine 150 na wafungwa wote wa kisiasa waachiliwe huru nchini Uturuki."

Kitisho cha SPD kuangukia nyuma ya AFP

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu uwezekano wa kutoweka katika medani ya kisiasa chama kikongwe kabisa cha kisiasa nchini Ujerumani SPD. Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika: "Uchunguzi wa maoni ya wananchi uliofanyika hivi karibuni unatisha-Unaonyesha wakitetereka kidogo tu, basi chama hicho cha Willy Brand, Helmut Schmidt na Gerhard Schröder kinaweza kuangukia nyuma ya AFD. Katika hali kama hiyo kimoja tu ndicho kilichowabakia: kujadiliana. Majadailiano yanayoendelea kusaka uungaji mkono wa makubaliano ya kuunda serikali ya muungano pamoja na CDU/CSU ni tiba inayofaa kwa chama hicho cha SPD."

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Saumu Yusuf