1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa umoja wa mataifa kuhusu usalama wa chakula waanza Rome.

Sekione Kitojo16 Novemba 2009

Mkutano wa kilele wa umoja wa Mataifa kuhusu suala la njaa duniani umeanza leo mjini Rome nchini Italia.

https://p.dw.com/p/KY5J
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon atahutubia mkutano wa chakula mjini Rome leo.Picha: picture-alliance/ dpa

Mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa kuhusu suala la njaa duniani umeanza leo katika mji mkuu wa Italia Roma. Mkutano huo utajadili kuhusu hatma ya watu zaidi ya billioni moja wanaokabiliwa na njaa duniani.Tayari wanaharakati wameonya kwamba mkutano huo huenda ukakosa maana kwasababu ya kutoshiriki kwa viongozi wa nchi tajiri za dunia.

Waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi ni kiongozi pekee kutoka kundi la nchi za G8 ambaye ni miongoni mwa viongozi wengine 60 wa nchi na serikali wanaoshiriki mkutano huo juu ya njaa utakaomalizika jumatano.Kiongozi wa kanisa katoliki duniani ni mmoja wa watu watakaouhutubia mkutano huo unaofanyika kwenye makao makuu ya shirika la chakula na kilimo duniani FAO mjini Roma.

Viongozi wengine ambao wanahudhuria mkutano huo ni rais wa Brazil Luiz Inacio Lula Da Silva,Moammar Kadhaffi wa Liya,Hosni Mubarak wa Misri,Hugo Chavez wa Venezuela na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Mashirika ya kibinadamu wiki iliyopita yalionya kwamba mkutano huo huenda ukawa wa kupoteza wakati kutokana na hatua ya viongozi wa nchi tajiri kutohudhuria na kutoa mwito wa kuwepo hali ya kujitolea kwa hali na mali katika kukabiliana na njaa duniani.Mashirika hayo ya kibinadamu ikiwemo shirika la madktari wasiokuwa na mipaka,yamezungumzia masikitiko yake juu ya hatua hiyo ya viongozi wa nchi tajiri.Shirika la Oxfam kwa upande wake limesema ni hali ya kusikitisha kuona kwamba nchi tajiri zinashindwa kuonyesha shauku na umuhimu juu ya suala hilo.Itakumbuikwa kwamba katika mkutano wa kundi la G8 katika kipindi cha msimu wa joto kilichpita nchi hizo ziliahidi kutoa dolla billioni 20 kwa ajili ya shughuli za kilimo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na ahadi hiyo imebakia kuwa hadithi.Akizungumza kuhusu hali ya njaa ilivyo duniani mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa mazingira UNEP Achim Steiner amesema-

''Si watu wengi wanatambua kwamba tunakabiliwa na matatizo ya usalama wa chakula duniani na pia upungufu wa chakula kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani,kwa upande mwingine ni wazi kwamba mifumo ya uzalishaji na uuzaji bidhaa za kilimo unapoteza kiasi cha asilimia 30 hadi 40 ya kila kinacholimwa.''

Kanisa Katoliki nchini Italia pia limeonya kwamba mkutano huo unaweza usifanikiwe ikiwa viongozi hawatokuwa na misimamo ya kujitolea kwa dhati. Muswaada wa azimio la mwisho linalotazamiwa kuidhinishwa katika mkutano huo haujazungumzia kuhusu dolla billioni 44 ambazo zimependekezwa na mkuu wa shirika la umoja wa mataifa la chakula na kilimo, FAO ,Jacques Diouf kutolewa kila mwaka kwa ajili ya kusimamia shughuli za kilimo katika nchi masikini.

Wiki iliyopita mkuu huyo wa FAO alitilia mkazo juu ya kulipa uzito suala la kukabiliana na njaa akisema kwamba kila sekunde sita kuna mtoto anayefariki kutokana na njaa. Aliongeza kusema kwamba janga hilo sio tu linasababisha hali ya kufadhaisha kimaadili na kuvuruga hali ya uchumi, lakini pia inaashiria kitisho kikubwa katika hali jumla ya amani na usalama duniani.

Robert Calderisi mfanyakazi katika ofisi ya benki ya duniani barani Asia na Afrika na pia amewahi kuandika kitabu kinachoitwa tatizo la Afrika,juu ya kulisaidia bara hilo katika kukabiliana na njaa kwa upande wake amesema-

''Jambo muhimu linalohitajika kufanywa barani Afrika na ambalo hakuna anayelishughulikia ni kuimarisha shughuli za kilimo.Kilimo ni utajiri mkubwa katika Afrika lakini ni suala lililopuuzwa au kutumiwa vibaya kwa muda mrefu na serikali za bara hilo juu ya suala la kodi na usaidizi ambao umekuwa ukitolewa kwa wakulima wadogo sio wakuridhisha''

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa ambaye atahudhuria kwa muda mfupi mkutano huo anatazamiwa kuwashinikiza viongozi wa dunia kuongeza juhudi katika harakati za kukabiliana na ongezeko la joto ulimwenguni pamoja na njaa. Kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo duniani FAO ,shughuli za uzalishaji bidhaa za kilimo zinabidi kuongezwa kwa asilimia 70 ikiwa ulimwengu unataka kumudu kuwalisha watu billioni 9 kufikia mwaka 2050.Mashirika yasiyo ya kiserikali pia yameandaa mkutano wake pembezoni mwa mkutano wa Roma.Mkutano huo unaotoa mwito wa kuweko uhuru wa chakula kwa kila mtu utahudhuriwa na mkuu wa FAO Diouf na meya wa jiji la Roma Gianni Alemanno.Hapo jana wakati wajumbe wakianza kukusanyika katika mji huo wa Roma benki ya Kiislamu ya mendeleo IDB ilitoa ahadi ya mapema ya dolla billioni moja kwa ajili ya kusimamia miradi ya pamoja na shirika la FAO.Zaidi ya wajumbe 400 kutoka nchi takriban 70 wanahudhuria mkutano huo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba (AFP)

Mhariri: Sekione Kitojo