Mkutano wa Umoja wa Afrika waanza leo mjini Addis Ababa
31 Januari 2008Zaidi ya viongozi 40 wa nchi za Afrika wanahudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.
Mkutano wa siku tatu wa umoja huo wenye wanachama 53 unaanza leo na unatarajiwa kujadili juhudi za amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan, machafuko yanayoendelea nchini Somalia na mada rasmi ya ujenzi wa viwanda.
Swala lengine litakalojadiliwa katika mkutano huo ni vipi kuishughulikia Kenya.
Shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka limeutolea mwito mkutano wa mjini Addis Ababa kuilaani na kuiwekea vikwazo Eritrea kwa kuwatesa wafungwa.
Shirika hilo limetoa mwito huo baada ya kuchapisha ripoti yake ikiilaumu serikali ya Eritrea kwa kutumia vitendo vya ukatili dhidi ya watu inaowaona kuwa hatari.
Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limemtaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amshinikize hadharani rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, akubali waranti wa kukamatwa kwa raia wawili wa Sudan wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur.
Ban Ki Moon atakutana na rais Bashir kandoni mwa mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa akiwa na matumaini ya kuondoa vikwazo dhidi ya jeshi la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika la kulinda amani Darfur.