1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Somalia waendelea Uturuki

Admin.WagnerD1 Juni 2012

Mkutano wa Kimataifa kuhusu Somalia uliendelea kwa siku ya pili Ijumaa Mjini Instanbul, Uturuki kujadili changamoto za kisiasa na kiuchumi zinazoikabili nchini hiyo ikiwa ni pamoja na muda wa mwisho wa serikali ya mpito.

https://p.dw.com/p/156JE
Rais wa Somalia Sharif Sheik Ahmed, Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Rais wa Somalia Sharif Sheik Ahmed, Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Somalia, Abdiweli Mohammed ameelezea matumaini ya nchi yake kuondoka katika hali mbaya iliyomo hivi sasa na kuwa na mchango muhimu kwa jumuiya ya kimataifa.

Katika taarifa yake iliyojaa matumaini aliyoisoma mbele ya mamia ya Wasomali na wajumbe kutoka kona mbalimbali duniani waliohudhuria mkutano huo, Waziri Mkuu huyo alisema Somalia ina mambo mengi mazuri kuliko uharamia, wanamgambo na njaa, na kuongeza kuwa Wasomali wanaweza kuifundisha dunia mambo kadhaa kuhusu uthabiti.

Waziri Mkuu wa Somali Mohamed Ali Abdiweli.
Waziri Mkuu wa Somali Mohamed Ali Abdiweli.Picha: Reuters

Matumaini ya kuwa na taifa bora
Ali ambaye alinusurika kuuawa katika mripuko wa bomu mwezi Aprili alisema anatumaini wakati unakaribia ambapo Somalia itaweza kutumia pwani yake ndefu na kunufaika na biashara kutoka kwa raia wake waliotapakaa duniani kote na kujenga uchumi imara unaoiungansha Afrika na Mashariki.

Aliongeza kuwa kwa sasa nchi yake inajaribu kuimarisha mafanikio yaliyopatikana dhidi ya kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa Al-qaeda.

"Tumefanikiwa kuudhibiti Mji Mkuu wa Mogadishu na maeneo mengi ambayo yalikuwa hayatawaliki katika mikoa ya kusini na kati ndani ya miezi tisa. Wanamgambo wa Al-Shabaab hawatadumu kwa muda mrefu. Mbinu zao chafu sasa zimewakosesha uungwaji mkono," alisema Ali.

Mkutano wa Istanbul uliohudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 54 uliendeshwa chini ya kauli-mbiu - 'Namna ya kujenga mustakabal bora.' Awali, akielezea malengo ya Mkutano huo, Waziri Mkuu huyo wa Somalia alisema:

"Tunataka kuielekeza Somalia katika mwanzo mpya, mbali kabisaa na dhana zilizozoeleka kama taifa lililoshindikana na kuirudisha katika enzi za taifa huru la kijivunia. Mkutano huu utakuwa wa mafanikio kama kama jamii ya kimataifa itatoka na msimamo mmoja juu ya mustakabali wa Somalia."

Ujumbe muhimu katika taarifa za ufunguzi wa Mkutano huo ulihusu haja ya kuwepo na juhudi zinazoungwa mkono na jamii ya kimataifa kuijenga upya Somali. Chanzo kimoja kutoka wizara ya mambo ya nje ya Uturuki kilisema agenda moja ilikuwa kuishinikiza Somalia kukubaliana na agenda ya kisiasa ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon naye alikuwepo katika Mkutano huo.
Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani kutoka Uganda.Picha: picture-alliance/ dpa

Masuala muhimu ya Mkutano
Siku ya kwanza ya mkutano huo ilikuwa inajadili maendeleo ambapo wafanyabiashara wa kisomali na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na waakilishi wa kisiasa kutoka Somalia na kimataifa walijadili mbinu za kuijenga upya nchi hiyo, wakielekeza zaidi nguvu kwenye ujenzi, nishati na maji. Lakini mfanyabiashara Abdirahman Abdiqan anasisitiza kuwa usalama bado ni jambo muhimu kwa maendeleo.

"Hakuna anaeweza kufanya baishara na hakuna mtu anaweza kufanya jambo lingine kama mazingira ya kisiasa siyo mazuri, ukosefu wa usalama. Haileti hata maana unapozungumzia msaada wa kiutu," alisema Abdiqan.

Agenda nyingine muhimu ya mkutano huu ni kuanzisha mfuko wa kimataifa kuwezesha kulipia mafunzo ya vikosi vya ulinzi na usalama vya Somalia. Siku ya pili ya mkutano huo ilijadili maandalizi ya kuhitimisha kipindi cha serikali ya mpito mwezi Agosti.

Mmoja wa waliohudhuria mkutano huo, Ibrahim Mahadale alisema mpango wa huu ambao utaielekeza Somali katika uchaguzi, ni muhimu sana kwa mustakabali wa nchi hiyo. " Kipaumbele ni namna ya kukamilisha mchakato huo kabla ya tarehe 20 Agosti, wana miezi 2 na natumai wanaweza kumaliza ndani ya muda huo. Changamoto kubwa ni namna ya kuchagua wabunge."

Wataalam wanasema kufanikisha mpango huo uliokubaliwa na viongozi wa Somali unaonekana kuwa mgumu. Lakini Waziri Mkuu Abdiweli Mohammed Ali anasema wanaendelea vizuri na majadiliano juu ya ukubwa wa bunge lijalo an kuhakikisha uwakilishi wa wanawake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE
Mhariri; Mohammed Abdul Rahman