1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Korea Kaskazini yupo tayari kukutana na Trump

Yusra Buwayhid
27 Mei 2018

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ataondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea na kuhudhuria mkutano wa Singapore Juni 12 wa kukutana  na Rais wa Marekani Donald Trump.

https://p.dw.com/p/2yPCV
Südkorea Nordkorea - Moon Jae-in und Kim Jong Un in Panmunjom
Picha: picture alliance/Xinhua News Agency/Blue House

Katika mkutano wa ghafla wa Jumamosi, Moon na Kim wamekubaliana kwamba mkutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini lazima ufanyike, kama Moon alivyosema katika mkutano wake na waandishi habari, mjini Seoul.

"Mimi na mwenyekiti Kim tumekubaliana kwamba mkutano wa kilele wa Juni 12 lazima ufanyike kwa ufanisi, na jitihada yetu ya kupatikana rasi ya Korea isiyo na silaha za nyuklia, na utawala wa amani wa kudumu haipaswi kusimamishwa," amesema Moon.

Rais wa Marekani Donald Trump kwa upande wake ameashiria kwamba maandalizi ya mkutano wa kilele wa Juni 12 yanaendelea, licha ya kuufuta mkutano huo wiki iliyopita.

Mkutano huo kati ya viongozi wa Korea mbili ni mabadiliko ya hivi karibuni, katika wiki iliyogubikwa na misukosuko ya kidiplomasia kuhusiana na mkutano wa kilele wa aina yake ambao haukuwahi kutokea kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

Treffen Regierungschefs Süd- und Nordkorea
Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in katika mkutano na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong UnPicha: picture-alliance/AP Photo/South Korea Presidential Blue House

Moon, aliyerudi mjini Seoul Alhamisi baada ya kukutana na Trump mjini washington, amesema amerusi na ujumbe imara kutoka kwa Trump wa kutaka kukomesha uhusiano wa chuki na Korea Kaskazini na badala yake kujenga uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Katika barua mabyo Trumo alimtumia Kim Alhamisi, kiongozi huyo alifuta mkutano huo wa kilele uliopangwa kufanyika Singapore, kwa kile alichokitaja "uhasama wa dhahir" unaoonyeshwa na Korea Kaskazini.

Hata hivyo, ilipofika Jumamosi Trump alisema kwamba bado anatarajia kuhudhuria mkutano wa kilele wa Juni 12 huko Singapore na kwamba matayarisho yanaendelea vizuri sana.

"Tunaendelea vyema kuhusiana na mkutano wa kilele na Korea Kaskazini," alisema Trump akiwa Ikulu ya Marekani, Whire House. "Matayarisho yanaendelea vyema. Kwahiyo tunautarajia mkutano wa Singapore wa Juni 12. Hilo halikubadilika. Kwa hiyo, tutaona kitakachotokea."

Timu ya ikulu ya Marekani itaelekea Singapore mwishoni mwa juma hili kama ilivyopangwa kwenda kufanya matayarisho ya mkutano huo wa kilele, kulingana na kauli ya Jumamosi ya msemaji mkuu wa ikulu ya Marekani.

Trump und Moon Jae In Washington
Donald Trump na Moon Jae-in wakiwa ikulu ya White House mjini Washington, Marekani Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Mitazamo tofauti juu ya suala la kuondoa nyuklia

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Jumapili katika taarifa yake iliyoituma katika shirika la habari la Reuters kwamba inatarajia mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa na kwa mafanikio, na kurudia wito wake wa kuzitaka pande zote mbili kuonyesha subira na nia njema.

"Tumekuwa na imani kuwa mawasiliano na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Marekani ni muhimu katika kutatua suala la nyuklia katika rasi ya Korea," imesema taarifa hiyo.

Huku akiwa anahakikisha kwamba Kim yupo tayari kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea, Moon amekiri Korea Kaskazini na Marekani zinaweza kuwa na matarajio tofauti juu ya maana hasa ya suala hilo. Kiongozi huyo wa Korea Kusini amezisisitiza pande zote mbili kufanya mazungumzo ya kistaarabu ili kutatua tofauti zao.

Afisa mwandamizi wa Korea Kusini amesema kabla ya kufayika mkutano kati ya Korea Kaskazini na Marekani, Korea hizo mbili zitajadiliana juu ya ahadi isiyo na vurugu na kuanzisha mazungumzo ya amani kama njia ya kushughulikia wasiwasi wa Korea Kaskazini wa suala la usalama wa nchi yake.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afp

Mhariri: John Juma