1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Rio+20 waanza

20 Juni 2012

Wanachama wa Umoja wa Mataifa katika mkesha wa Mkutano wa Kilele wa Maendeleo Endelevu unaofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil wameunga mkono mpango wa kutunza mazingira na kujenga uchumi utakaozingatia mazingira.

https://p.dw.com/p/15IH0
Mwanamke akipita kwenye alama ya Mkutano wa Rio+20, Brazil.
Mwanamke akipita kwenye alama ya Mkutano wa Rio+20, Brazil.Picha: Reuters

Lakini faraja ya kuepusha kushindwa kwa mkutano huu ili usije kuwa kama yale yaliotokea katika Mkutano wa Kilele wa Tabia Nchi mjini Copenhagen Denmark hapo mwaka 2009, kumechanganyika na hali ya kukatisha tamaa kwa wengi, ambao wanaona makubaliano hayo ni muafaka wa kuhuzunisha.

Kamishna wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Umoja wa Ulaya Corinie Hedegaard amesema hakuna mtu aliefurahia kupitishwa kwa rasimu ya azimio hilo na kila mmoja anajuwa kwamba azimio hilo ni dhaifu.

Baada ya kuzozana kulikodumu hadi usiku wa manane wajumbe wa mataifa wametowa idhini ya awali kwa rasimu ya waraka huo wa kurasa 53 uliobuniwa kutumika kama dira kwa maendeleo endelevu katika kipindi cha muongo mmoja na kuendelea.

"Mustakabali Tuutakao"

Waraka huo uliopewa jina la " Mustakbali Tunaoutaka " unataja hatua za kupambana na matatizo mengi ya mazingira yanayoikabili dunia na kuwatowa mabilioni ya watu kwenye dimbwi la umaskini kwa kwa kupitia sera ambazo zitatunza mali asili badala ya kuzivuruga.

Vikosi vya usalama vikilinda mkutano wa Rio+20.
Vikosi vya usalama vikilinda mkutano wa Rio+20.Picha: DW

Mataifa duniani yatatowa ahadi ya kujenga mustakbali endelevu kiuchumi,kijamii na kimazingira duniani kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Rasimu ya waraka huo inatarajiwa kuidhinishwa na viongozi wa dunia hapo Ijumaa kuufunga mkutano huo wa siku 10 wa Maendeleo Endelevu.

Viongozi wa dunia wameanza kuwasili mjini Rio de Janeiro kwa ajili ya mkutano huo unaoanza Jumatano tarehe (20/06/2012) ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa nchi au serikali takriban mia moja kutoka nchi 193 duniani. Juhudi za miezi kadhaa zimetumika kuwekeza kwenye mradi huo.

Mataifa na makundi ya kanda yamekuwa yakizozana juu ya namna ya kuendeleza uchumi unaotunza mazingira, kukusanya fedha kusaidia ukuaji wa uchumi usiochafuwa mazingira katika nchi za kimaskini na kutowa ufafanuzi juu ya mpango wa '' Malengo Endelevu" ambao utachukuwa nafasi ya mpango wa "Malengo ya Maendeleo ya Milinia ya Umoja wa Mataifa" baada ya kumalizika muda wake hapo mwaka 2015.

Kuna mengi ya kufanywa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil, Antonio Patriota ,amewashukuru washiriki kwa mchango wao kufuatia mazungumzo ya usiku kucha mjini Rio de Janairo na kusema kwamba wana maudhui yaliokubaliwa kwa asilimia 100. Umoja wa Ulaya ulitowa wito wa mazungumzo hayo kurefushwa kutokana na kutofurahishwa na maudhui ya rasimu ya azimio hilo.

Washauri wa Mkutano wa Rio+20.
Washauri wa Mkutano wa Rio+20.Picha: DW

Mwenyeji wa mkutano huo Brazil iliingilia kati kutafuta usuluhishi wa pamoja baada ya washiriki kushindwa kufikia muafaka ili kwamba azimio la mwisho liweze kusainiwa katika mkutano huo.

Rasimu ya azimio hilo imeepuka maamuzi muhimu kama vile uanzishaji wa mfuko wa maendeleo endelevu halikadhalika mfumo wa taasisi ya dunia kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na mataifa.

Uhusiano kati ya Rio+20 na Maendeleo ya Milenia

Brice Lalonde, waziri wa zamani wa mazingira wa Ufaransa, ambaye ni mratibu wa mkutano huo amesema anaamini Malengo ya Maendeleo Endelevu yanaweza kuibuka kama nyota katika mkutano huo. Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba malengo hayo yataziathiri nchi zote za kitajiri na kimaskini.

Mameya wanaoshirikia mkutano wa Rio+20.
Mameya wanaoshirikia mkutano wa Rio+20.Picha: dapd

Mkutano huo wa Maendeleo Endelevu unafuatilia ule uliofanyika miaka 20 iliopita ambao ni Mkutano wa Kilele wa Mazingira Duniani ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilianzisha hatua za kuzuwiya mabadiliko ya tabia nchi,kuenea kwa jangwa,kutoweka kwa viumbe hai na umaskini.

Mkutano huo utahudhuriwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini pamoja na Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh, na mwenzake wa China, Wen Jiabao.

Rais Barack Obama wa Marekani hatohudhuria mkutano huo na atawakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje. Hilary Clnton. wakati Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron. ambao pia hawatohudhuria mkutano huo. wanawakilishwa na mawaziri wao mazingira.

Takriban wanaharakti 50,000, wakurugenzi watendaji wa biashara na watengeza sera wanahudhuria mkutano huo. Wataalamu wengi wanaamini kwamba matukio yanayofanyika pembezoni mwa mkutano huo yana tija zaidi kiutendaji kuliko hata azimio la kisiasa linalotarajiwa kutolewa hapo Ijumaa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman