Mkutano wa OIC waanza Cairo
6 Februari 2013Mkutano huo unamuweka rais wa Misri Mohammed Morsi katika nafasi ya juu huku kukiwa na mtikisiko wa kisiasa na kiuchumi nchini mwake.Wakati huo huo rais wa Iran anaizuru Misri ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mkutano huo.
Wakati rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad akifanya ziara ya kwanza nchini Misri kufanywa na kiongozi wa Iran , baada ya miaka 34 ya mtengano, mkutano huo wa siku mbili utalenga zaidi juu ya njia ya kusitisha mauaji nchini Syria, nchi ambayo ni mshirika pekee wa rais Bashar al-Assad katika eneo hilo.
Tamko la pamoja
Tamko la pamoja lililotayarishwa na mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa 56 wanachama wa shirikisho la ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu, OIC, na kupatikana na shirika la habari la reuters, linatoa lawama kwa serikali ya Assad kwa mengi ya mauaji hayo na kuitaka serikali hiyo kuanzisha mazungumzo kuhusu kipindi cha mpito cha kisiasa.
Tamko hilo pia limeidhinisha na kutambua muungano wa upinzani wa kitaifa nchini Syria, na kuutaka kuharakisha kuundwa kwa serikali ya mpito, ambayo itakuwa tayari kuchukua madaraka kamili hadi pale yatakapofikiwa mabadiliko kamili ya kisiasa yanayohitajika.
Rasimu hiyo ya waraka , ambayo inaweza kufanyiwa mabadiliko wakati wa mkutano huo , inatoa wito wa kupatikana suluhisho litakaloelekezwa na Wasyria wenyewe katika mzozo huo, ambapo kiasi ya watu 60,000 wamepoteza maisha hadi sasa na rasimu hiyo ina kataa uingiliaji kati kutoka mataifa ya kigeni.
Bila ya kumtaja Assad, rasimu hiyo inasema, " Tunauhimiza utawala wa Syria kuonyesha busara na kuitisha mjadala ambao utafanyika baina ya wawakilishi wa baraza la muungano wa kitaifa , majeshi ya upinzani, na wawakilishi wa serikali ya Syria ambao wana nia ya dhati ya kufanya mageuzi ya kisiasa nchini Syria pamoja na wale ambao hawajahusika moja kwa moja kwa njia yoyote ile katika kuwakandamiza watu".
Ombi la mazungumzo
Kiongozi wa baraza la muungano wa kitaifa SNC, Moaz Alkhatib alitoa ombi mwishoni mwa juma la kukutana na makamu wa rais Assad , Farouq al-Shara, kwa ajili ya mazungumzo ya amani iwapo maafisa watawaacha huru maelfu ya wafungwa .
Rais wa Misri Mohammed Mursi , ambaye ni mwanachama wa chama cha udugu wa Kiislamu, atataka kuionyesha nchi yake kuwa ni kiongozi wa mataifa ya Kiislamu wakati atakapofungua mkutano huo , miezi saba tangu kuwa kiongozi wa kwanza wa taifa la Misri aliyechaguliwa kidemokrasia.
Wakati rais Mahmoud Ahmedinejad akifanya ziara yake ya kwanza nchini Misri katika muda wa miaka 34, kiongozi wa ngazi ya juu wa dini ya Kiislamu nchini Misri amemwambia kiongozi huyo wa Iran kutoingilia kati katika masuala ya ndani ya Bahrain na mataifa mengine ya eneo la ghuba, na pia kulinda haki ya waumini wachache wa madhehebu ya Sunni nchini mwake.
Ahmed al-Tayyeb imamu mkuu wa msikiti wa Al-Azhar na chuo hicho kikuu mjini Cairo , pia ameshutumu kile alichokieleza kuwa ni kusambaa kwa Ushia katika mataifa ya waumini wa Kisunni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman