Viongozi wa NATO wanaendelea na mkutano wao.
4 Aprili 2009STRASBOURG.
Viongozi wa nchi za jumuiya ya kijeshi ya Nato leo wanaendelea na mkutano wao unaofanyika kuadhimisha mwaka wa 60 wa jumuiya yao.
Mkutano huo uliokirimiwa kwa pamoja baina ya Ujerumani na Ufaransa umezingatia mkakati mpya wa Marekani juu ya Afghanistan.Marekani inazitaka nchi nyingine nazo za jumuiya ya nato zichangie majeshi zaidi na misaada kwa ajili ya Afghanistan.
Mapema leo katika hatua ya kuonesha moyo wa Umoja, rais Obama wa Marekani, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani , rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na viongozi wengine walivuka daraja linalozitenganisha Ujerumani na Ufaransa.Wakati huo huo Ufaransa imerejea kikamilifu katika jumuiya hiyo ya kijeshi.
Habari zaidi kutoka kwenye mkutano wa viongozi wa nato zinasema viongozi hao wameshindwa kumchagua katibu Mkuu mpya wa jumuiya yao baada ya mjumbe aliekuwa na uwezekeno mkubwa, wa kuchaguliwa ,waziri mkuu wa Denmark kupingwa na Uturuki.Uturuki imemlaumu waziri mkuu huyo bwana Anders Fogh Rasmussen kwa jinsi alivyoshuhgulikia mzozo juu ya kukashifiwa mtume wa dini ya kiislamu- Mohammed.
Marekani imesema hakuna haja ya kuwa na haraka katika suala hilo.Katibu mkuu wa hadi sasa bwana Jaap de Hoop Scheffer anajiuzulu mwishoni mwa mwezi julai.Habari zaidi zinasema polisi leo walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuwazuia wapinzani kufika kati kati ya mji wa Strasbourg ambapo mkutano unafanyika.