1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa NATO

Munira Mohammad3 Aprili 2009

Rais Barack Obama tayari amewasili nchini Ufaransa, kuhudhuria mkutano wa NATO. Viongozi wa jumuiya NATO wanakutana huko Strassbourg na Baden Baden kwa maadhimisho ya miaka 60 tangu kubuniwa kwa NATO.

https://p.dw.com/p/HPTx
Katibu mkuu wa NATO, Jaap de Hoop SchefferPicha: picture-alliance/dpa
EU Gipfel in Brüssel Angela Merkel und Nicolas Sarkozy
Kansala wa Ujerumani Angela Markel na Nicholas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: AP

Utakuwa mkutano wa kwanza wa NATO kwa rais Barack Obama na pia itakuwa nafasi ya kuikaribisha tena Ufaransa iliyokuwa imejiondoa katika jumuiya hiyo. Marekani inatarajiwa kuwasilisha mkakati wake mpya kuhusu Afghanistan na kuzitaka nchi zingine ziongeze wanajeshi Afghanistan.

Mwenyeji wa mkutano huu wa siku mbili ni Ujerumani na Ufaransa, inayotoa sura ya maridhiano baada ya vile vita baridi. Lakini maafisa wa NATO walikuwa wepesi wa kusema huu si wakati wa sherehe.

Rais Obama kwanza atafanya mkutano na mwenyeji wake Nicholas Sarkozy. Kisha ataelekea Baden Baden, mji wa mpakani ya Ufaransa na Ujerumani kwa mkutano na Kansela wa Ujerumani Angela Markel. Shughuli rasmi ya mkutano huu itaanza leo jioni.

Quiz Obama Merkel
Merkel na Obama

Kulingana na maafisa wa NATO katibu mkuu wa jumuiya hiyo Jaap Hoop Scheffer ananuia mkutano huu kujadili maswala muhimu na kupata maafikiano. Ajenda muhimu zitazojadiliwa ni pamoja na uhusiano wa jumuiya hiyo na Urusi ambao umekuwa na mvutano. Mchango wa NATO nchini Afghanistan pia utajadiliwa. Rais Barack Obama anasemekana atawasilisha mkakati wake mpya kuhusu Afghanistan wiki moja tu baada ya kutangaza kupeleka majeshi 4,000 Afghanistan.

Akizungumza kabla ya mkutano huu Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alisema Washington inatarajia nchi wanachama wa NATO wataahidi kuchangia hali nchini Afghanistan kwa kutoa wanajeshi, pesa na wataalam kupiga jeki juhudi za Marekani kukabiliana na hali tete nchini Afghanistan.

Katibu mkuu wa jumuiya ya NATO Jaap De Hoop Scheffer alisema ana imani swala la Afghanistan litapata jawabu la kufaa katika mkutano huo.

''Pengine si Nato tu lakini pia umoja wa ulaya pamoja na jumuiya nyingine zenye nguvu zinaweza kufanya mengi zaidi kutokana na kutofurahishwa na hali iliyokuwepo na ya wakati huu kwa hivyo tuna nafasi nzuri kwamba leo au kesho kutapatikana uamuzi wa viongozi wa serikali ya kuwepo mkakati mpya bila shaka ni jambo litakalochukua wakati lakini tuna uhakika kabisa uamuzi huo utapatikana.'' Alisema De hoop Scheffer kuhusiana na swala la Afghanistan.

Rais wa Albania na waziri mkuu wa Croatia pia watafika kwa mara ya kwanza baada ya mataifa yao kujiunga rasmi na jumuiya ya NATO.

Urusi ambayo imekuwa na uhusiano wa mvutano na NATO tayari imeonya kuhusiana na swala la kufungulia milango nchi zingine kujiunga na NATO. Urusi inapinga vikali kujumuishwa kwa mataifa ya Ukraine na Georgia.

Na kama ilivyokuwa mjini London katika mkutano wa nchi tajiri duniani wa kundi la G-20. Waandamanaji pia wamo katika miji hii miwili mwenyeji wa mkutano huu wa NATO. Mjini Strasbourg, Ufaransa polisi tayari wamewakatama waandamanaji 300, baada ya makabiliano makali. Ulinzi mkali umeimarishwa katika eneo la mkutano. Mji wa Baden Baden Ujerumani pia polisi wameweka ulinzi kuzuia machafuko yeyote katika mkutano huuu wa NATO.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFP

Mhariri: Josephat Charo