Mawaziri washindwa kuafikiana.
7 Machi 2008
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za mfungamano wa kijeshi -NATO wameshindwa kuafikiana juu ya kuwaingiza wanachama wapya katika mfungamano wao lakini viongozi wa nchi hizo watakutana tena mwezi ujao mjini Bukarest.
Utata ulitokea kwenye mkutano huo kutokana na Ugiriki kupinga Mecccedonia kuingizwa katika mfungamano huo kutokana na nchi mbili hizo kuzozana juu ya jina hilo Maccedonia. Ugiriki inasema kwa Maccedonia kutumia jina hilo maana yake ni kutoa madai juu ya sehemu yake ya kaskazini yenye jina kama hilo.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za mfungamano wa kujihami-NATO kwenye mkutano wao pia walijadili uanachama wa Albania na Croatia.
Ugiriki imesema haina kipingamizi juu ya nchi hizo mbili. Lakini ilitishia kutumia kura ya veto kuzuia Maccedonia kupewa uanachama wa NATO.
Mawaziri wa NATO, pia walitafakari uwezekano wa Ukraine na Georgia kuingizwa katika uanachama wa mfungamano wao.
Lakini Ujerumani na Ufaransa zimeeleza mashaka juu ya hayo. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa bwana Kouchner amewaambia wandishi habari kuwa nchi yake inazingatia kuwa ni jambo muhimu sana kwa Umoja wa Ulaya kuendeleza uhusiano mzuri na Urusi.
Hatahivyo katibu mkuu wa NATO Jaap
de Hoop Scheffer amesisitiza umuhimu wa NATO katika kudumisha amani barani Ulaya.
Viongozi wa nchi na serikali wa madola ya Nato wanatarajiwa kukutana mjini Bukarest Rumania mwezi aprili ambapo masuala hayo yatatazamiwa kujadiliwa.