Mkutano wa NATO wakamilika kwa kuzikemea China na Urusi
15 Juni 2021Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo wa siku moja mjini Brussels, viongozi wa NATO wameelezea kwa matamshi makali wasiwasi wao kuhusu tabia za China wanazosema zinakwenda kinyume na maadili ya jumuiya hiyo pamoja na sheria za kimataifa.
Taarifa yao imeanisha kuwa malengo ya China na tabia ya taifa hilo la Kikomunisti ni changamoto kubwa linapokuja suala la ushirikiano duniani chini ya kanuni za kimataifa.
Wasiwasi mkubwa mkubwa ulioelezwa na mataifa wanachama wa Jumuiya hiyo ni pamoja na kuimarika kwa uwezo wa kijeshi wa China, uhusiano kati ya nchi hiyo na Urusi pamoja na kile walichokitaja kuwa kukosekana uwazi mjini Beijing.
Ama kuhusu Urusi, wanachama wa NATO hususani mataifa ya Baltiki na nchi zinazopakana na Urusi zimesema bado zinaizingatia Moscow kuwa kitisho cha usalama.
China na Urusi zawa ajenda muhimu za mkutano
Suala la China na Urusi limepata nafasi ya juu kwenye mkutano wa NATO kutokana na uwepo wa rais Joe Biden wa Marekani ambaye amehudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza akinuwia kuimarisha tena mahusiano yaliyolegalega kati ya Washington na washirika wake wa magharibi.
Rais Biden ambaye amepangiwa kukutana na rais Vladimir Putin wa Urusi siku ya Jumatano mjini Geneva amesema atamweleza kinagaubaga kuwa Washington haitosita kujibu iwapo Moscow itaendeleza tabia zake za ubabe.
Biden amesema Jumuiya ya NATO ni sharti isimame imara dhidi ya kitisho kinachoongezeka kutoka Beijing na Moscow.
"Maadili ya demokrasia yaliyo kitovu cha ushirika wetu yanakabiliwa na mbinyo wa ndani na wa nje. Urusi na China zote zinajaribu kuukaba koo mshikamano wetu wa magharibi. Lakini ushirika wetu ni msingi imara ambao tunaweza kuutumia kujenga ulinzi wa pamoja na ustawi imara." amesema Biden.
Lakini ni rahisi kuitenga China kimataifa?
Licha ya matamshi makali yaliyotolewa kuhusu China, viongozi kadhaa wa mataifa ya Jumuiya ya NATO wamesema bado ni muhimu kushirikiana na Beijing katika masuala mengi duniani ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Biden mwenyewe ni miongoni mwa wale wanaoamini kuwa siyo rahisi kuitenga moja kwa moja China katika uga wa kimataifa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema China, taifa kubwa na lenye nguvu za kiuchumi duniani ni hasimu kwenye maeneo mengi lakini wanakubali kuwa Beijing bado vilevile ni mshirika muhimu katika masuala chungunzima.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikwenda mbali zaidi akisema hakuna anayetaka "kutumbukia kwenye vita vipya baridi na China" lakini ni muhimu kudhibiti changamoto zinazotokana na matendo ya Beijing.
Hata hivyo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron yeye amewatahadharisha viongozi wenzake kutopotea njia kwa kuacha kutekeleza dhima ya msingi ya jumuiya ya NATO na kutumia muda mwingi kushughulika na China ambaye amesema ina nafasi ndogo mno kwenye masuala ya pamoja ya washirika wa NATO.