Mkutano wa NATO kuhusu Georgia
16 Septemba 2008
Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO, Jaap de Hoop Scheffer amezungumzia uungaji mkono wa jumuia hiyo kwa Georgia wakati wa mkutano wa kwanza wa kamisheni ya Nato na Georgia ulioitishwa jana mjini Tblissi.Hata hivyo katibu mkuu de Hoop Scheffer hakutaja tarehe ya kujiunga Georgia na jumuia ya NATO.
Kilikua kikao cha kwanza kabisa cha kamisheni ya pamoja ya Georgia na jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO iliyoundwa baada ya Urusi kuivamia Georgia mwezi uliopita.
Viongozi wa Tblissi wanauangalia mkutano huo kama ishara ya uwezekano wa kukubaliwa uanachama wa NATO,ingawa maombi yao bado hayaungwi mkono na wanachama wote wa jumuia hiyo.
Waziri mkuu wa Georgia Lado Gurgenidse anasema:
"Ni tukio la kihistoria.Ni hatua ya maana kwa Georgia.Hatua ya kuelekea kujiunga Georgia na Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO."
Katika wakati ambapo kamisheni ya pamoja ya NATO na Georgia ilikua ikikutana mjini Tblissi,mjini Brussels nako walikutana mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa ulaya kuzungumzia uwezekano wa kutumwa tume ya Umoja huo nchini Georgia.Mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wametangaza msaada wa hadi yuro milioni 500 kwa Georgia hadi ifikapo mwaka 2010.
Akifungua kikao cha Tblissi,Jaap de Hoop Scheffer amesema jumuia ya NATO inaamini bado kwamba jibu la Urusi kwa uamuzi wa Georgia wa kutuma wanajeshi Ossetia ya kusini,mwezi uliopita,lilikithiri.Ameitolea mwito Urusi itekeleze vifungu vyote 6 vya makubaliano yaliyofikiwa kutokana na upatanishi wa rais Nicholas Sarkozy wa ufaransa.
Hata hivyo katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,hakwenda umbali wa kutamka kama Georgia itapatiwa kanuni maalum za kuweza siku moja kujiunga na jumuia hiyo.Bwana Jaap de Hoop Scheffer anasema hatua hiyo itategemea jinsi shughuli za kamisheni ya pamoja ya NATO na Georgia zitakavyofanikiwa.Kamisheni hiyo imepewa jukumu la kuisaidia Georgia katika kuleta mageuzi yanayohitajika kabla ya kujiunga na NATO.
"Kuna mambo muhimu ambayo Georgia inabidi iyatekeleze.Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa NATO watakutana December ijayo kuzungumzia vifungu hivyo."
Nchi za magharibi zinaishinikiza Georgia iimarishe mfumo wa kidemokrasi na kuendeleza mageuzi.
Balozi wa Marekani katika NATO,Kurt Volker,ambae nchi yake imepania kuiona Georgia ikikubaliwa uanachama na jumuia ya NATO,nae pia ameonyesha kukubaliana na hoja za walio wengi.
"Uamuzi wa kupatiwea Georgia kanuni maalum utapitishwa baadae" amesema bwana Kurt Volker.
Katika wakati ambapo katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO alikua ziarani mjini Tblissi,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov alikwenda Ossetia ya kusini jana,baada ya ziara ya hapo awali huko Abkhasia,huku rais Dmitri Medvedev akitoa onyo kwa mara nyengine tena mjini Moscow dhidi ya nchi za Magharibi.