Mkutano wa mwaka wa Shirika la Mazingira la Umoja wa mataifa wapokea ripoti kuhusu janga la Tsunami.
23 Februari 2005Mkutano wa mwaka wa Shirika la mazingira la umoja wa mataifa –UNEP, ukiwa ni wa 23, unaendelea katika makao makuu ya Shirika hilo mji huo mjini Nairobi-Kenya, wakati ripoti ya umoja wa mataifa ikisema nchi zilizokumbwa na janga la Tsunami, hazina kujenga vizuizi vya kimaumbile katika kingo zao za pwani, kujilinda na majanga ya aina hiyo mnamo siku zijazo.
Uoteshaji miti na hasa mivinje karibu na kingo za pwani, ni jambo litakalosaidia kupunguza athari za majanga aina ya Tsunami na mengineyo. Itakumbukwa kwa janga hilo Desemba 26 mwaka jana 2004, liliwauwa karibu watu 290,000 katika maeneo ya bahari ya hindi.
Ripoti ya umoja wa mataifa inasema kipa umbele hakina budi kuwa ni katika kuendeleza misitu kwenye maeneo ya pwani, kwani miti itasaidia kuzuwia nguvu za tsunami nyengine sdiku zijazo, pamoja na mmomonyo wa ardhi, kwa sababu ya kupanda kwa vina vya bahari na pia kufikia malengo ya kitaifa ya uoteshaji upya wa misitu na kufungua nafasi za ajira.
Ripoti hiyo iliopewa jina la* Baada ya Tsunami-tathmini ya haraka ya Mazingira*- imetolewa katika mkutano wa mwaka wa Shirika la mpango wa Mazingira la umoja wa mataifa (UNEP) unaoendelea mjini Nairobi.
Shirika hilo linakadiria kwamba gharama za ujenzi mpya na makaazi mapya kwa walioathirika zitafikia dola bilioni 10 na kuchukua muda wa miaka hata 10 kuukamilisha mpango huo.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Klaus Töpfer alisema kuna sababu chungu nzima za kulinda na kudumisha vitu kama matumbawe, sehemu ambazo ni muhimu kwa samaki na kivutio kwa watalii.
Kadhalika pametolewa wito kuzitaka nchi husika ziondowe ujenzi wa majengo karibu na maeneo ya pwani katika mipango yao, hasa katika zile sehemu ambazo ni shida kuzuwia mawimbi makubwa na mafuriko. Nchi zilizoathirika kutokanana Tsunami,hazina budi kuwa mfano kwa kuchukua hatua za kutenga maeneo ya hoteli na utalii katika sehemu zilizo mbali na maeneo ya hatari.
Kwa upande mwengine ripoti ya Umoja wa mataifa imesema kwamba taka taka za sumu kutokana na janga ala Tsunami zinatoa kitisho kikubwa kwa afya za wakaazi wa nchi zilizoathirika. Imeripotiwa nchini Somalia kwa mfano kumezuka visa vya watu kutoka damu mdomoni, matatizo ya kupumua na hata ya ngozi. Maeneo ya mwambao nchini Somalia yamekua yakitumiwa kuwa ni maeneo ya kumwaga taka za kinuklea na sumu nyengine kwa miaka mingi sasa, kutokana na vita virefu vya wenyewe kwa wenyewe na ukosefu wa serikali huku kukiwa hakuna ukaguzi wala njia za kuzuwia ujambazi wa aina hiyo.
Hayo yametokana na ripoti hiyo iliokua ikitathimini athari za kimazingira, zilizosababishwa na janga la Tsunami kama serikali za Sri Lanka, Thailand, Indonesia, Maldive, Seychelles, Yemen na Somalia zilivyoliomba Shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa mataifa.. Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Bw Töpfer alisema utafiti umefafanua ju ya athari za Tsunami katika sekta mbali mbali za maeneo hayo na matatizo yanayohitaji hatua za haraka.