1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa muungano wa BRICS wajadili utanuzi

23 Agosti 2023

Mkutano wa kilele wa BRICS umeingia siku ya pili Jumatano (23.08.2023) Johanesburg, Afrika Kusini. Nchi wanachama zinapania kuimarisha ushawishi kuukabili muundo wa uchumi wa dunia unaoongozwa na nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/4VU3L
Südafrikas Präsident Cyril Ramaphosa bei dem BRICS-Gipfel
Picha: Sergei Bobylev/imago images/ITAR-TASS

Viongozi wa muungano wa BRICSwamegeukia ajenda kuu ya mkutano wao, siku moja baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kuzikosoa nchi za magharibi. Muungano huo unajadili uwezekano wa utanuzi na kuruhusu wanachama wapya wajiunge, ikiwa ni zaidi ya muongo mmoja tangu ulipoasisiwa. Zaidi ya nchi 20 zimewasilisha rasmi maombi ya kutaka uanachama ikiwemo Saudi Arabia.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amezikosoa mara kadhaa nchi za magharibi katika hotuba yake kwenye mkutano huo kwa njia ya video kuhusu kile alichokiita kuwa ni vikwazo visivyo halali dhidi ya nchi yake na akatishia kukatisha kabisa usafirishaji wa nafaka ya Ukraine. Hotuba yake ya dakika 17 ilijikita juu ya vita vya Ukraine na mahusiano baina ya Urusi na nchi za magharibi, licha ya kwamba maafisa wa Afrika Kusini walikuwa wameshauri misuguano kati ya ukanda wa mashariki na magharibi wa dunia isipewe nafasi kuugibika mkutano huo wa BRICS ambapo viongozi wanakutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu janga la corona kuzuka.

Putin beim BRICS Summit
Rais wa Urusi, Vladimir PutinPicha: Mikhail Klimenty/imago imsges

"Tunashirikiana kwa msingi wa kanuni za usawa, kusaidiana katika ushirikiano, heshima kwa maslahi ya kila mwanachama, na huu ndio msingi muhimu wa muelekeo wa kimkakati wa siku za usoni wa muungano wetu, mkondo unaokidhi mahitaji na kutimiza malengo ya sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa." Putin alisema.

"Katika muongo mmoja uliopita, uwekezaji wa pamoja wa nchi wanachama wa BRICS umeongezeka mara sita. Kutokana na hilo uwekezaji wao katika uchumi wa dunia kwa ujumla umeongezeka maradufu, na thamani jumla ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hizo imefikia asilimia 20 ya kiwango jumla cha dunia." Putin aliongeza.

Soma zaidi: Mkutano wa jumuiya ya BRICS waanza rasmi Johannesburg

Putin hakusafiri kwenda Johannesburg kuhudhuria mkutano wa BRICS, badala yake anapanga kushiriki kwa njia ya mtandao. Anawakilishwa kwenye mkutano huo na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov.

BRICS haina nia ya kushindana na G7 wala G20

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva alisema jana Jumanne kwamba muungano wa BRICS haulengi kupingana na muungano wa nchi zilizostawi kiviwanda duniani wa G7 wala muungano wa nchi zilizostawi kiuchumi na zile zinazoinukia kwa kasi kiuchumi za G20. Lula alisisitiza kwamba BRICSinapania kuweka msingi mzuri wa ushirikiano wa ukanda wa kusini wa dunia. Lula alisisitiza kuwa wanachama wa BRICS ni muhimu katika mdahalo wa dunia na wanataka kukaa pamoja katika meza ya mazungumzo wakiwa katika ngazi sawa na Umoja wa Ulaya na Marekani.

BRICS Summit in Johannesburg
Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da SilvaPicha: Gianluigi Guercia/Reuters

Rais wa China Xi Jinping pia alitoa kauli akisema kuna nchi moja inayotaka kuendeleza masilahi yake na imeelekeza nguvu nyingi katika kukwamisha masoko yanayoinukia na nchi zinazoendelea duniani. Katika hotuba yake iliyowasilishwa na waziri wa biashara wa China, Xi aidha alisema nchi yoyote inayokua kwa kasi kiuchumi na yoyote inayoikaribia dola hiyo, inalengwa na kukwamishwa. Alikuwa akizungumzia msuguano kati ya Marekani na China.

Rais Xi yuko Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa BRICS na alikutana jana na rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa, lakini hakuhudhuria kikao cha ufunguzi. Hakuna sababu iliyotolewa.

Muungano wa BRICS, unaozijumuisha Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini ulianza mkutano wake wa siku tatu jana Jumanne unaotarajiwa kutuwama juu ya utanuzi wake, kuzijumuisha nchi nyingine kadhaa kama wanachama wapya. Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, mwanamfalme Faisal bin Farhan na rais wa Iran Ebrahim Raisi wanatarajiwa kuhudhuria kikao cha leo.

(ap, dpa)