Mkutano wa Merkel na Sarkozy mjini Berlin
15 Juni 2010Ujerumani na Ufaransa zimeweka kando tofauti zao za maoni kuhusu sera za siku za mbele za fedha za Umoja wa Ulaya .Hali hiyo imewezekana kutokana na mkutano wa jana kati ya kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, mjini Berlin.
Kimsingi, Nicolas Sarkozy alitaka kuja Berlin tangu wiki moja iliyopita, lakini ziara hiyo iliakhirishwa kwa ghafla. Duru zinasema hali hiyo ilisababishwa na hitilafu za maoni kati ya rais wa Ufaransa na kansela wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani kuhusu sera za fedha za Umoja wa Ulaya. Jana jumatatu, viongozi hao wawili wakaondoa hitilafu zao za maoni. Sikwambii tena hawakutaka kujitokeza katika mkutano ujao wa kilele wa Umoja wa ulaya kama kizingiti, bali wanataka waendelee kuangaliwa kama injini ya Umoja wa Ulaya. Nicolas Sarkozy amedokeza mazungumzo yao hayakua rahisi-lakini mwishoe,yeye na Merkel wameridhika:Kansela Angela Merkel amesema:
"Ahsante Nicolas, kwa kuja huku kwetu. Ninahisi kwamba Ujerumani na Ufaransa tumebainisha tunaweza na kwamba hata mustakbal wa Umoja wa Ulaya tunaweza kuusimamia."
Maridhiano yaliyofikiwa yanazungumzia juu ya umuhimu wa kukubaliana nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya linapohusika suala la sera za kiuchumi na sio peke yao nchi 16 za zoni ya Euro kama Sarkozy alivyopendekeza. Alitaka iundwe taasisi maalum ya kushughulikia masuala ya kiuchumi, mfano wa serikali ya kiuchumi- hakufanikiwa lakini kumtanabahisha kansela Angela Merkel aunge mkono fikra hiyo.
Uwezekano wa kupatikana ufumbuzi unakutikana kutokana na hoja kwamba pindi ikihitajika, basi serikali 16 za zoni ya sarafu ya Euro ziwajibike tuu ikiwa maridhiano yatashindikana kati ya mataifa 27.
Mgogoro wa Ugiriki umebainisha jinsi utaratibu kama huo ulivyo muhimu. Nicolas Sarkozy ameonyesha kuridhika na maridhiano yaliyofikiwa hata kama Paris haikupata taasisi mpya ya kushindana na benki kuu ya Ulaya, kama viongozi wa Ufaransa walivyokua wakitaka.
Viongozi hao wawili, kansela Angela Merkel na rais Nicholas Sarkozy, wameshauri pia pawepo utaratibu wa kuwekewa vikwazo nchi yoyote ile ya Umoja wa Ulaya ambayo haitoheshimu mpango wa kuhakikisha utulivu wa bajeti. Vikwazo hivyo ni pamoja na kupokonywa haki ya kupiga kura nchi husika. Kama kutakua na haja ya kubadilishwa sheria za Umoja wa Ulaya ili kutekeleza pendekezo hilo, suala hilo litajibiwa wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya alkhamisi ijayo mjini Brussels.
Mwandishi: Werkhäuser, Nina(DW Berlin)Hamidou,Oummil
Mpitiaji: Miraji Othman