1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mazingira Paris waingia wiki muhimu ya mwisho

Admin.WagnerD8 Desemba 2015

Mawaziri waliopewa jukumu la kupatikana mkataba wa kihistoria kuiokoa dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi katika mkutano wa Umoja wa mataifa mjini Paris wamekuwa wakijaribu kutatua maeneo yanayosababisha mivutano.

https://p.dw.com/p/1HJLE
Frankreich Klimagipfel in Paris Ban Ki-moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon , katika mkutano wa ParisPicha: Reuters/S. Mahe

Maeneo hayo yanayosababisha mivutano ,ni kama vile udhibiti wa mabilioni kadhaa ya dola yatakayoelekezwa kusaidia mataifa yanayoendelea.

Mazungumzo hayo ya Umoja wa mataifa yanayohusisha mataifa 195 yanaonekana kuwa fursa ya mwisho ya kuepusha athari mbaya za kupanda kwa ujoto duniani, ikiwa ni pamoja na ukame uliokithiri, mafuriko na vimbunga, kupanda kwa viwango vya maji ya bahari ambayo yanatishia kuvimeza visiwa na maeneo ya pwani yanayokaliwa na watu wengi.

Frankreich Klimakonferenz COP21 Paris Demonstration
Wanaharakati wa mazingira wakionesha bango linalotaka kutangazwa "hali ya hatari ya mazingira" katika mkutano wa ParisPicha: Reuters/E. Gaillard

Kufikia makubaliano hayo ambayo mara kadhaa yanaponyoka ifikapo muda wa mwisho siku ya Ijumaa, hata hivyo, mawaziri hao kwanza lazima watatue mizozo kadhaa iliyodumu kwa miongo mingi ambayo imezuwia njia ya kupatikana mkataba wa kwanza wa kweli kuhusu mazingira.

Tofauti bado zipo

Mataifa bado yanatofautiana juu ya vipi yatatoa msaada wa fedha kwa mataifa yanayoendelea ili kumudu athari za kupanda kwa ujoto duniani, ni kwa kiasi gani kupunguza sayari yetu kupata joto zaidi, vipi kugawana mzigo baina ya mataifa tajiri na mataifa masikini, na vipi itawezekana kufanya mapitio ya hatua zilizopigwa katika kupunguza gesi zinazochafua mazingira.

Mazungumzo hayo yamepata kasi tangu jana , ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alizitaka serikali za mataifa mbali mbali kuanzisha kile alichokieleza kuwa ni "mapinduzi ya nishati" ili kudhibiti utoaji wa gesi zinazobeba joto zinazoharibu mazingira na kuepusha ongezeko la ujoto duniani.

Äthiopien Dürre Kinder skelettierte Rinder
Ukame nchini EthiopiaPicha: picture-alliance/dpa/J. Robine

Umoja wa Ulaya unaonekana kulegeza msimamo wake kuhusu madai kwamba malengo ya upunguzaji wa gesi hizo katika makubaliano ya mkutano wa Paris yawe yanashurutisha kisheria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema kwamba hata kama makubaliano hayo hayatalazimisha kisheria, lakini makubaliano bado yataweza kubadili jinsi ulimwengu wa kibiashara unavyofikiri juu ya nishati.

Bahari ni sehemu ya mfumo wa maisha

Ameongeza kwamba ni lazima dunia ijaribu kupunguza hali ya ujoto ili kuokoa viumbe baharini , kwa kuwa bahari ni sehemu muhimu ya maisha yetu.

Israel Totes Meer Trockenheit Verdunstung Küste
Viwango vya maji ya bahari vinapandaPicha: Getty Images/AFP/M. Kahana

"Bahari imo katika hatari. Bahari ni mfumo unaohusiana na maisha. Na bahari inahitaji kulindwa kama maeneo mengine ya maisha yetu katika sayari hii. Na pamoja na ukubwa wake na uzuri wake, imo katika hatari. Na ndio sababu niko hapa leo. Na ndio sababu mko hapa leo, na haiwezi kuwa muhimu zaidi ya hivyo."

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito wa kupata mapinduzi ya nishati salama ili kuepuka , kile alichosema , "maafa ya kimazingira" wakati mazungumzo hayo ya mjini Paris yakiingia katika wiki yake ya mwisho.

Deutschland Bundesumweltminsterin Barbara Hendricks im Bundestag
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara HendricksPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Bara la Afrika litapewa dola bilioni 10 kulisaidia kujenga vyanzo vya nishati endelevu, wakati Ujerumani ikiongoza nchi tajiri katika mchango wake.

Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks amesema hayo jana pembezoni mwa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa mjini Paris.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / ape

Mhariri: Yusuf, Saumu