1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO mjini Noordwijk

Oummilkheir24 Oktoba 2007

Afghanistan ni miongoni mwa mada moto moto zitakazojadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili

https://p.dw.com/p/C7gR
Mwanajeshi wa NATO mjini Kabul nchini Afghanistan
Mwanajeshi wa NATO mjini Kabul nchini AfghanistanPicha: AP

Mawaziri wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wanakutana baadae hii leo kwa mkutano wa siku mbili mjini Noordwijk nchini Uholanzi.Mzozo wa Afghanistan ni miongoni mwa mada muhimu zitakazojadiliwa.

Katika kikao cha siri,mara baada ya mkutano huo wa siku mbili kufunguliwa leo jioni huko Noordwijk,mawaziri wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO watazungumzia kinaga ubaga kasoro zilizoko ndani ya jumuia yao pamoja pia na namna ya kusawazisha hali hiyo.

Afghanistan ndio mada inayoendelea kuishughulisha jumuia ya NATO.Wakuu wa kijeshi walioko nchini humo,hawatachoka kudai wanajeshi waongezwe,vifaa vizidishwe na kutaka pia pawepo waalimu zaidi kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Afghanistan .Lakini kutokana na kitisho kinachowakabili wanajeshi,baadhi ya mataifa yanachama wa NATO yanajizuwia na hasa panapohusika na kutumwa wanajeshi katika maeneo ya hatari kusini mwa Afghanistan.Mataifa yaliyotuma wanajeshi katika maeneo hayo,kwa mfano Marekani,Uengereza na Canada yamekua yakilalamika na kudai na mataifa mengine pia yawajibike katika maeneo hayo.

Mzozo sugu unaonyesha kuripuka kati ya washirika wawili wa NATO.Uturuki inajipa haki ya kuhujumu maeneo ya kaskazini ya Irak ili kuwavunja nguvu wanamgambo wa kikurd.Wamarekani hawavutiwi hata kidogo na msimamo huo.Wanahofia mtafaruku usije ukaenea hata katika yale maeneo ya UIrak ambayo hadi wakati huu yalikua salama.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates,amewatolea mwito waturuki wajizuwie:

“Opereshini kubwa ya kijeshi kaatika eneo la mpakani,ni dhidi ya masilahi ya Uturuki,dhidi ya masilai yetu na dhidi ya masilahi ya Irak.”

Japo kama Uturuki inaonyesha kuregeza kamba,lakini haikuondowa uwezekano wa kushambulia.

Mzozo mwengine unaotokota ni kuhusu mipango ya Marekani ya kutega mitambo ya kufyetulia makombora katika nchi za Ulaya mashariki,ili iweze kwa mfano kuzuwia makombora yatakayovurumishwa na Iran.Hadi wakati huu Robert Gates hakufanikiwa katika juhudi zake za kuwatanabahisha viongozi wa Urusi mjini Moscow kuhusu mtambo huo ambao viongozi wa Urusi wanauangalia kua ni kitisho kwao.Hata nchini Poland na katika jamhuri ya Tcheki wananchi hawauangalii kwa jicho jema mpango huo wa Marekani.Katika nchi hizo ndiko Marekani inakopanga kutega baadhi ya mitambo hiyo.

Katika wakati ambapo mataifa hayo mawili ya kambi ya zamani ya mashariki ,yameshajiunga na jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,mataifa matatu ya Balkan,Albania,Kroatia na Mazedonia zinasubiri kukubaliwa uanachama.Nato lakini inahimiza mageuzi zaidi yafanywe katika nchi hizo.

Mada nyengine itakayojadiliwa mjini Noordwijk ni kuhusu kikosi cha kuingilia kati haraka.Hata katika suala hilo misimamo inatofautiana miongoni mwa mataifa wanachama wa NATO.