1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO mjini Krakow wajadili mageuzi.

Sekione Kitojo20 Februari 2009

Katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa NATO nchini Poland hali imefahamika kuhusu ni wanajeshi wangapi wa ziada watapelekwa.

https://p.dw.com/p/GxxR
Mawaziri wa ulinzi wa NATO kabla ya mkutano wao mjini Krakow nchini Poland.Picha: AP


Katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa NATO nchini Poland upelekaji wa wanajeshi wa ziada nchini Afghanistan umefahamika, kiasi cha wanajeshi 17,000 kutoka Marekani na 600 kutoka Ujerumani.


Kwa Poland, ambayo ndio mwenyeji wa mkutano huu baada ya miaka kumi ya kuwa mwanachama wa NATO, pia ni suala la hadhi kubwa. Hali ya usalama nchini Afghanistan ambayo inazidi kuporomoka inapelekea NATO kutoweza kuwa katika hali ya furaha. Na baada ya miaka kadha ya mapambano katika nchi hiyo hali haijabadilka nchini humo.

Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza kuwa wanajeshi wa Marekani 17,000 watapelekwa nchini Afghanistan. Hatua hiyo inawatupia mpira mataifa mengine washirika. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Jung aliyeko mjini Krakau amejibu kwa kusema.

Naikaribisha hatua ya Marekani kupeleka wanajeshi wa ziada, hususan katika suala la kuimarisha hali ya usalama katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan. Kuimarisha usalama , kwa hiyo, nahisi ni suala muhimu. Lakini tusiangalie tu upande wa usalama , badala yake tunahitaji tuangalie pia kuendeleza kwa upana kuhakikisha kuwa usalama unapatikana , lakini pia ujenzi wa jamii.


Hata hivyo, waziri Jung hazungumzii suala hili akiwa mikono mitupu. Ujeruamni itatuma wanajeshi wa ziada 600 nchini Afghanistan, ambapo baadhi yao watashiriki katika kulinda usalama wakati wa uchaguzi nchini humo unaotarajiwa kufanyika August mwaka huu.

Wakati huo huo, Jung anahisi kuwa utawala mpya wa rais Obama utatilia maanani kwa kiwango sawa baina ya matumizi ya nguvu za kijeshi, ujenzi wa jamii pamoja na elimu, na kwamba ataelekeza katika kile kinachoitwa mtazamo mpaka.

Lakini NATO pia ina tatizo kubwa la kuaminika. Kutokana na taarifa za umoja wa mataifa kwa mwaka ulipita pekee karibu raia elfu moja wameuwawa na ama majeshi ya serikali ya Afghanistan ama na wanajeshi wa mataifa ya nje. Katibu mkuu wa NATO Hoop Scheffer anasema kuwa majeshi ya washirika wanafanya kila liwezekanalo kuepuka makosa hayo.

Kwa bahati mbaya, naweza kusema haiwezekani kuepuka kabisa wahanga, lakini napenda kusema kuwa sijawahi kukutana na sitaweza kabisa kukutana na mwanajeshi mmoja wa NATO ama wa jeshi la washirika ambaye atanuwia kwa maksudi kuua raia wasio na hatia. Nia ya kuua raia wasio na hatia kwa maelfu ni nia waliyonayo wapiganaji wanaotupinga, ni nia waliyonayo Taliban na sio NATO.


Wakati huo huo, mawaziri wa ulinzi wa NATO wanalenga katika kuleta mageuzi katika umoja huo ili kusaidia kuweza kupambana na vitisho vya hivi sasa pamoja na nia ya Georgia na Ukraine, mataifa ambayo nia yao ya kutaka kuwa wanachama wa NATO, imezidisha hali ya wasi wasi baina ya mataifa ya magharibi na Urusi.