Mkutano wa mawaziri wa nje wa NATO
5 Machi 2009Shirika la Ulinzi la Magharibi (NATO), katika kikao chake cha mawaziri wa nje mjini Brussels,Ubelgiji hii leo ,linatazamiwa kuungamkono juhudi za kurejesha mahusiano rasmi na Urusi huku Marekani na washirika wake , wakijitahidi kuwa na mshikamano mkubwa zaidi katika vita vya kupam,bana na watalibani nchini Afghanistan.
Katika kikao cha leo, waziri wa nje wa Marekani bibi Hillary Clinton,ataelezea maendeleo katika mkakati mpya wa utawala wa rais Barack Obama wa kuikagua upya mbinu ya kufuatwa huko Afghanistan.
Shirika la ulinzi la NATO linaloongozwa na Marekani lilisimamisha ushirikiano wake na Moscow baada ya Urusi kuivamia Georgia August mwaka jana,lakini timu ya rais Obama huko Ikulu mjini Washington, imebainisha wazi kabisa kwamba ina azma ya kufungua ukurasa mpya katika usuhuba wake na Urusi.
Wakati wakisisiza kwamba bado kuna mvutano na wasi wasi kuhusu vitendo vya Urusi.maafisa wa Marekani na NATO , wamesisitiza hatahivyo, masilahi ya pamoja yaliopo baina yao na Moscow hasa katika kupambana na itikadi kali ya kiislamu na hata wasi wasi kuhusu mradi wa kinuklia wa Iran.
Inatazamiwa kama matokeo ya kikao cha leo mjini Brussels, kupitishwa uamuzi wa kuanzishwa upya mikutano ya kupitisha maamuzi ya lile Baraza la pamoja kati ya NATO na Urusi (NRC).
Katika kikao cha leo kinachohudhuriwa kwa mara ya kwanza na waziri wa nje Bibi Clinton, mbali na Urusi,Afghanistan na vita dhidi ya wataliban itachukua sehemu kubwa.Marekani inataka kuutumia upepo mpya uliovuma ulaya juu ya shauku kubwa kwa Rais Barck Obama, ili kuungwamkono kwa njia ya kujitolea washirika wa NATO wa ulaya kuchangia vikosi zaidi nchini Afghanistan.
Marekani imeamua kuongeza askari 17.000 nchini Afghanistan wakati Ujerumani ambayo tayari ina vikosi vyake huko itachangia askari 600 zaidi. Holland inatazamia pia kupeleka askari zaidi nchini Afghanistan kuitikia hodi hodi za Rais Obama.
Waziri wa nje wa Marekani Hillary Clinton akitumai kuufufua usuhuba uliochafuka na
Moscow,atakuwa na mazungumzo ya kwanza marefu na waziri mwenzake wa nje wa Urusi Sergei Lavrov,mjini Geneva hapo kesho ijumaa. Swali la kudhibiti silaha linatazamiwa kuwa kileleni mwa ajenda yao na hasa swali la kutegwa makombora huko Ulaya ya Mashariki na kwa kadiri gani Urusi yaweza kuibembeleza Iran kuachana na mradi wake wa kinuklia.
Hatahivyo, Washington inadai haijaribu kufukia kabisa tofauti zake na Moscow na hivyo, itaendelea na msimamo wake wa kutotambua eneo la ushawishi inalopigania Moscow kluwa nalo huko Ulaya ya mashariki:Wala haitautambua uhuru wa maeneo yaliojitenga na Georgia.Isitoshe, Marekani inashikilia uzi wake ule ule kuwa nchi za Ulaya kama vile Ukraine na Georgia, zina uhuru wa kuomba uwanachama wa NATO-jambo ambalo linaikasirisha Kremlin.