1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa NATO mjini Brussels

Oumilkher Hamidou15 Oktoba 2010

Ujerumani inapigania Urusi ijumuishwe katika mpango wa kinga dhidi ya hujuma za makombora kutoka nchi adui mfano Iran

https://p.dw.com/p/Per6
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani (kushoto) Guido Westerwelle na mwenzake wa ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg mkutanoni mjini BrusselsPicha: picture alliance/dpa

Tunaelekea mjini Brussels ambako mawaziri wa mambo ya nchi za nje na wale wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO wametoa ishara ya kufikia maridhiano ya kuunda mfumo wa pamoja wa kinga dhidi ya makombora barani Ulaya.

"Makubaliano yako karibu sana kufikiwa",amesema hayo waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Karl-Theodor zu Guttenberg pembezoni mwa mkutano huo mjini Brussels.Wakati huo huo akaunga mkono fikra ya kujumuishwa Urusi katika mpango huo.

Mkakati wa ulinzi ulioanzishwa miaka 11 iliyopita wakati mawaziri wa mambo ya nchi za nje na wenzao wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO walipokutana,umepitwa na wakati hivi sasa anasema waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Karl-Theodor zu Guttenberg.

"Mkakati mpya unahitajika haraka kwasababu huu wa sasa misingi yake ni ya tangu mwaka 1999 na tangu wakati huo ulimwengu umebadilika na mambo mengi yamejitokeza ambayo NATO inabidi iyazingatie."

Miongoni mwa mambo hayo ni ugaidi ulioenea ulimwenguni ambao ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabili jumuia ya NATO,lakini pia kitisho cha kutokea hujuma dhidi ya mitandao ya internet, au kuzimwa vinu vya nishati au mitambo viwandani.

Brüssel NATO Anders Fogh Rasmussen Belgien
Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO,Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Katibu mkuu wa wa jumuia ya kujihami bya NATO,Anders Fogh Rasmussen amejaribu pia,licha ya makasha matupu, kuwatanabahisha washirika juu ya umuhimu wa kuwa na mpango wa pamoja wa kinga dhidi ya makombora.Hata hivyo kauli ya mwisho inatazamiwa kutamkwa viongozi wa taifa na serikali watakapokutana mjini Lisbonn November mwaka huu.

Mpango wa kinga dhidi ya makombora umelengwa kwa mfano kujikinga dhidi ya makombora kutoka Iran.Mpango huo unazusha mabishano hata miongoni mwa wajerumani.

Serikali kuu ya Ujerumani inataka kuwatanabahisha washirika wake juu ya umuhimu wa kupunguza silaha za kinuklea na kwa namna hiyo kuepukana pia na silaha zilizosalia za Marekani katika ardhi ya Ujerumani..Hata hivyo nchi nyingi zinashaka shaka.Kwa mfano Ufaransa inayohofia isije ikalazimika kuteketeza silaha zake za kinuklea.

Katika mipango ya kupunguza matumizi, jumuia ya kujihami ya NATO inafikiria kupunguza idadi ya wafanyakazi katika shughuli za utawala.Hata idadi ya makao makuu na wafanyakazi watapunguzwa kwa thuluthi moja.

Vituo gani vitahusika na hatua hizo,bado haijulikani.

Mwandishi: Hasselbach,Christoph (DW-Brüssel)/hamidou,Oummilkheir

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman