1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

mkutano wa mawaziri wa kujihami wa NATO mjini Nice -Ufaransa

oummilkheir10 Februari 2005

Mawaziri wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wanaokutana katika mji wa mwambao ,kusini mashariki ya Ufaransa Nice nchini, wamezungumzia njia za kuimarisha harakati mbali mbali zinazosimamiwa na jumuia hiyo nchini Irak na Afghanistan,katika wakati ambapo serikali ya Washington inawatia kishindo washirika wake wa Ulaya wazidi kuwajibika.

https://p.dw.com/p/CEGa
mawaziri wa NATO wakutana mjini Nice
mawaziri wa NATO wakutana mjini NicePicha: AP

Mkutano huu wa Nice,wa kwanza wa aina yake katika ardhi ya Ufaransa,nchi iliyojitenga na uongozi wa pamoja wa kijeshi wa jumuia hiyo tangu mwaka 1966,unafanyika katika hali ya kujaribu kutuliza mambo katika uhusiano kati ya Marekani na nchi zanachama za NATO barani Ulaya,baada ya mfarakano uliosababishwa na kujiingiza Marekani na Uengereza nchini Iraq katika mwaka 2003.

Mkutano huo unafanyika pia siku moja baada ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi 26 zanachama wa NATO kukutana mjini Brussels,na wiki mbili kabla ya mkutano wa kilele wa NATO february 22,pale viongozi watakapomkaribisha rais wa Marekani George W. Bush.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld amewatanabahisha mawaziri wenzake juu ya umuhimu wa uchaguzi wa Irak,january 30 iliyopita,akishauri nchi zote zanachama wa NATO zishiriki katika juhudi za kuvipatia mafunzo vikosi vya usalama vya Iraq.

Nchi kadhaa za ulaya zimejibu na kuahidi kusaidia.

"Wakati wa mazungumzo ya jana mjini Brussels,na haya ya leo mjini Nice,nchi kadhaa zimejitokeza na mapendekezo mepya" amesema msemaji wa jumuia ya kujihami ya magharibi James Appathurai,bila ya kuyataja ni mapendekezo ya aina gani.

Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO imeanzisha mpango wa kuwapatia mafunzo maafisa wa kijeshi wa Iraq-wakiwemo wakufunzi kama mia moja hivi.Nchi kadhaa zikiwemo Ufaransa,Ujerumani na Ufaransa kwa mfano zinatoa mafunzo hayo lakini nje ya Iraq.Lengo ni kuwapatia mafunzo maafisa kama elfu moja hivi wa Iraq kwa mwaka.

Ujerumani imeshaanza kuwapatia mafunzo maafisa wa kiiraq katika nchi za Emirati na Ufaransa imependekeza kuwapatia mafunzo gendarmes 1500 nchini Qatar.Pendekezo hilo la Ufaransa halijajibiwa lakini bado na viongozi wa mjini Baghdad.

Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO Jaap de Hoop Scheffer anasema lengo ni kuona ahadi zote zinakamilika hadi mkutano wa kilele wa NATO utakapoiitishwa february 22 ijayo.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Peter Struck anasema hakuna mvutano wowote kati ya wanachama wa NATO na watu wanashukuria mafunzo Ujerumani inayowapatia wanajeshi wa Iraq.

Mkutano wa Nice utakamilisha pia mipango ya kupanuliwa harakati za NATO hadi magharibi ya Afghanistan.

Mkutano huu wa Nice utamalizika kwa mawaziri wa ulinzi wa NATO kukutana na waziri mwenzao wa Rashia Serguei Ivanov kwa kile kinachojulikana kama baraza la NATO na Rashia.

Alipoufungua mkutano huo waNice leo asubuhi,waziri wa ulinzi wa Ufaransa bibi Michèle Alliot-Marie alisema" kwa kuukaribisha mkutano huo,Ufaransa imedhihirisha inabeba kikamilifu dhamana zake ndani ya NATO."