Mkutano wa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya
28 Novemba 2010Mawaziri wa Fedha wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo mjini Brussels, Ubelgiji kujadili kuhusu mkopo wa dharura wenye thamani ya Euro bilioni 85, kwa ajili ya Ireland inayokabiliwa na madeni makubwa. Jana umoja huo uliamua kuongezea hadhi mkutano huo iliokuwa umepangwa kufanyika kwa njia ya simu na kuufanya kuwa wa dharura na wa ana kwa ana.
Majadiliano kati ya maafisa wa Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na serikali ya Ireland yamekuwa yakiendelea kwa karibu wiki moja sasa mjini Dublin. Jana kiasi watu 50,000 waliandamana katika mitaa ya mji mkuu wa Ireland, Dublin, kupinga dhidi ya hatua mpya za nchi hiyo kubana matumizi.
Ili iweze kupatiwa msaada huo wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya na IMF, mapema wiki hii Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen, alitangaza hatua kali za kupunguza matumizi ya bajeti ya mwaka ujao wa 2011. Hatua hizo kali zinazopingwa zinajumuisha kupunguza mishahara, kuongeza kodi na kupunguza ajira 25,000 katika sekta ya umma.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE,RTRE)
Mhariri: Mohamed Dahman