1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa maji mjini Stockholm

9 Septemba 2010

Ulimwengu unakabiliwa na changamoto kubwa

https://p.dw.com/p/P7jG
Baadhi hutegemea maji machafu ambayo ni chanzo cha .Picha: AP

Mkutano wa wiki nzima wa wiki ya maji duniani uliofunguliwa siku ya Jumatatu katika mji mkuu wa Sweden umetoa tahadhari , kwamba muda unakwenda mbio kuliko upatikanaji wa maji salama.Iwapo changamoto tete na kubwa , zinazokabili moja kati ya mali asili muhimu sana hazitatafutiwa suluhisho hivi karibuni, hali ya baadaye inaonekana kuwa mbaya . Uhaba, uchafuzi, ukame, mafuriko, majangwa na magonjwa yatasambaa.

Gunilla Carlsson , waziri wa ushirikiano wa kimataifa wa Sweden , aliyaeleza mafuriko ya hivi karibuni nchini Pakistan kuwa moja kati ya maafa makubwa ya asili yanayoikabili nchi hiyo. Tuna wasi wasi mkubwa juu ya hali ya Pakistan , amesema , kuhusiana na nchi hiyo ambayo zaidi ya miaka 60 ya maendeleo ya miundo mbinu imeharibiwa kabisa katika maafa hayo yanayohusiana na mafuriko katika majimbo yaliyoathirika.

Alisema kuwa serikali ya Sweden hadi sasa imetuma kiasi cha dola milioni 20 kama msaada nchini Pakistan.Carlsson amesema kuwa sehemu ambazo zimeathirika mno , kama katika matukio mengi ya maafa ni kwa watu wasikini na jamii ya watu ambao hawajiwezi.

Katika hesabu ya mwisho, zaidi ya watu 1,700 wamefariki na zaidi ya nyumba milioni 1.2 pamoja na shule zimeharibiwa na mafuriko hayo, kwa mujibu wa ripoti kutoka Pakistan. Carlsson amesema inawezekana kuwa watu wengi zaidi wamefariki kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji, hata wakati Pakistan ikijitahidi kupambana na maafa hayo.

Akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa mkutano huo katika mji huo ambao umezungukwa na maji , Anders Berntell, mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kimataifa ya maji mjini Stockholm, ameonya kuwa maji machafu yanauwa watu zaidi kuliko ugonjwa wa ukimwi, malaria na vita vikichanganywa pamoja, na kuathiri maisha ya familia kadha pamoja na maendeleo ya kiuchumi ya nchi nyingi duniani.

Mkutano huo unaohudhuriwa na zaidi ya wataalamu muhimu 2,500 una angalia kauli mbiu inayosema kuangalia changamoto za dunia, changamoto ya ubora wa maji.

Huu ni mwaka 20 tangu taasisi hiyo ianze kuitisha mkutano huo na kuufanya mkutano huo wa wiki ya maji katika mji ambao unaelezwa kuwa mji wa kwanza katika bara la Ulaya unaofuata utaratibu ambao hauchafui mazingira.

Mwaka huu Berntell, amesema kuwa utaratibu wa majira umekuwa ukibadilika sana. Hatuwezi kusema kuwa matukio tofauti yaliyokuwa yakitokea ni athari za mabadiliko ya hali ya hewa, lakini utaratibu huu unaingiliana na mambo ambayo sayansi imeyatabiri. Kuanguka kwa kiasi kikubwa cha barafu, mafuriko pamoja na ukame mkubwa, amedokeza.Amesikitika kuwa wawakilishi wengi kutoka Pakistan hawakuweza kuhudhuria katika mkutano huo.

Katika majadiliano ya kimataifa kuhusu maji, kuna hali ya kulenga zaidi katika upatikanaji wa maji, lakini sio ubora. Maji machafu yanaathiri maisha ya binadamu pamoja na utendaji wa mfumo wa viumbe hai katika njia hiyo hiyo kama ukosefu wa maji, amesema Berntell.

Kwa mujibu wa tathmini ya milenia ya mfumo wa viumbe hai, amesema kuwa mfumo wa viumbe hai wa maji baridi umeharibika zaidi kuliko mifumo mingine ya viumbe hai, ikiwa ni pamoja na misitu ya mvua ya maeneo ya tropiki.

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya aina za samaki pamoja na viumbe wengine wanaoishi majini wako katika hatari ya kutoweka.Mkutano huo unamalizika Ijumaa Agosti 10.

Mwandishi: Sekione Kitojo / IPS

Mhariri : Abdul Rahman