Mkutano wa Mabadiliko ya tabianchi warefushwa Katowice
15 Desemba 2018Ukipangwa kumalizika Ijumaa, mkutano huo wa kilele COP24 mjini Katowice unafuata desturi na kurefushwa angalao hadi baadae Jumamosi baada ya mpango wa kuchapishwa mswaada wa maridhiano kuakhirishwa mara kadhaa.
Lengo ni kusaka njia za kutekeleza makubaliano ya Paris yaliyohimiza hali ya ujoto ipunguzwe kwa nyuzi joto mbili au 1.5.
Mivutano kati ya nchi za kaskazini na kusini inakorofisha juhudi za kufikiwa maridhiano. Kwa mujibu wa makubaliano ya Paris ahadi za nchi kupunguza moshi wa sumu ni za khiari. Lakini utekelezaji wake unabidi uwe wa uwazi na kuzihusisha nchi tofauti. Suala linalozuka ni vipi mataifa hayo yanaweza kuhimizwa yaonyeshe matokeo ya juhudi zao hadi ifikapo mwaka 2020?
Suala la fedha pia kugharimia hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi linazishughulisha nchi maskini za kusini na hasa kuhusu namna nchi za kaskazini zinavyopanga kuongeza kiwango cha fedha hizo kuanzia mwaka 2025.
Kundi la mataifa yanayoinukia na yale yaliyoendelea kiviwanda ikiwa ni pamoja na Ujerumani limetoa wito wa matumaini
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amelazimika kurejea Katowice jana, kwa mara ya tatu tangu mkutano huo ulipoanza, ili kujaribu kuzitanabahisha pande zinazohusika kuhusu umuhimu wa kufikiwa makubaliano.
Mataifa yanayokutana Katowice yameamua mkutano wa COP 25 ufanyike mwishoni mwa mwaka 2019 nchini Chile, baada ya Brazil kujitoa katika makubaliano ya Paris, tangu Jair Bolsonaro mkosoaji mkubwa wa hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/Afp
Mhariri: Buwayhid, Yusra