Mafashisti mamboleo wawasili mjini Cologne.
19 Septemba 2008
Wajumbe wenye itikadi kali za kibaguzi wameanza kuwasili leo mjini Cologne kuhudhuria mkutano wa kupinga hasa ujenzi wa msikiti katika mji huo.
Wajumbe hao kutoka sehemu mbalimbali za bara la Ulaya wanahudhuria mkutano huo uliotayarishwa na chama cha kinachopinga kuenezwa kwa uislamu .
Habari zinasema polisi wengi wamepelekwa katika mji wa Cologne ili kuzuia mapambano baina ya wabaguzi hao na watu wanaowapinga.
Mkutano huo umeandaliwa na chama kinachopinga kinachoitwa kuenea kwa dini ya kiislamu.
Wakati huo huo mamia ya watu walishikama mithili ya mnyororo mbele ya sehemu ambapo msikiti unatarajiwa kujengwa, katika sehemu ya Ehrenfeld, kupinga mkutano wa wawakilishi wa itikadi kali za mlengo wa kulia.
Meya wa sehemu hiyo, Josef Wirges
ameushutumu mkutano huo.
Akizungumzia juu ya harakati za kupinga mkutano wa wabaguzi, mbunge wa chama SPD kwenye bunge la mji wa Cologne Lale Akgün amesema jitihada hizo zinaonesha kuwa mji wa Cologne umesimama wima dhidi ya mafashisti mamboleo.
Jumuiya ya waislamu wa kituruki inayojenga msikiti huo imesema maandamano ya kupinga mkutano wa wabaguzi yamethibitisha mtazamo wa stahamala miongoni mwa wakaazi wa mji wa Cologne ambapo watu wa nasaba mbalimbali za kitamaduni wanaishi.
Hatahivyo meya mkuu wa mji huo Fritz Schramma amesema stahamala huondoka ikiwa mipaka fulani inavukwa. Ameeleza kuwa ameshiriki katika maandamano ya kupinga mkutano wa mafashisti mamboleo kwa sababu mji wake hautaki kuona mkutano kama huo.
Chama kinachojiita kuwa kinatetea maslahi ya watu wa mji wa Cologne Pro Cologne kimewaalika mafashisti mamboleo kuhudhuria mkutano unaoanza kesho katika mji huo ,kwa lengo la kupinga wanachoita kuenezwa uislamu.
Mafashisti mamboleo wanapanga kufanya mkutano mkubwa wa hadhara hapo kesho mjini Cologne
Wawakilishi wa makanisa,vyama vya wafanyakazi na asasi za kiraia pia wanajiandaa kupinga mkutano huo.
Katibu mkuu wa baraza kuu la waislamu nchini Ujerumani bwana Aiman Maziyek amewataka waislamu wote washiriki katika harakati za kupinga mkutano huo ,leo na kesho katika mji wa Cologne
Kamishna wa masuala ya wahamiaji nchini Ujerumani bibi Maria Böhmer pia ametoa mwito wa kupinga mkutano wa mafashisti mamboleo unaotarajiwa kuanza kesho mjini Bonn.