Mkutano wa kupambana na ufisadi waanza London
12 Mei 2016Mkutano huwa wa kilele unakuja siku chache, baada ya Cameron kuzitaja Nigeria na Afghanistan kuwa ni nchi zilizo na ufisadi mkubwa. Kauli iliyomkasirisha rais wa Nigeria Muhammadu Buhari.
Aidha miongoni mwa waliohudhuria mkutano huwo ni wawakilishi wa mataifa 50 tofauti, akiwamo waziri wa mmabo ya nje wa Marekani John Kerry pamoja na marais wa Afghanistan na Nigeria. Nchi ambazo Cameron alizitaja kuwa huenda zikawa zilizokithiri katika rushwa duniani.
Cameron alisikika akiyasema hayo kwenye vidio iliyonaswa bila ya mwenyewe kujua, alipokuwa akimuelezea Malkia wa Uingereza Elizabeth kuhusu mkutano huwo na viongozi wa mataifa ya dunia.
Cameron anatarajiwa kutangaza katika mkutano huwo kuwa makampuni yote ya kigeni yanayomiliki mali nchini Uingereza, yatalazimika kuweka wazi umiliki wa kampuni hizo katika daftari maalumu la umma litakalozinduliwa mwezi ujao. Hayo ni kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa ofisi ya Cameron.
"Naamini kwamba rushwa ni kansa inayosababisha matatizo mengi tunayokabiliana nayo duniani kote. Kama tunataka kuziona nchi zinaepukana na umasikini na zinapata utajiri, tunahitaji kupambana na ufisadi. Kama tunataka kuziona nchi zenye rasilimali kubwa , zinafanikiwa kuzitumia kwa manufaa ya raia wao, basi pia tunahitaji kupambana na ufisadi," amesema Cameron katika mkutano huwo.
Usajili wa makampuni ya kigeni waungwa mkono
Aidha ofisi ya Cameron imesema Ufaransa, Uholanzi, Nigeria pamoja na Afghanistan pia zitashiriki katika kuzindua madaftari ya umma ya kuandikisha umiliki wa kweli wa makampuni.
Na kuongeza Australi, New Zealand, Jordan, Indonesia, Ireland pamoja na Georgia zimekubali kuchukuwa hatua za awali, kueleka makubaliano hayo ya kuwa na daftari la umma la kusajili umiliki wa makampuni.
Cameron amesema daftari hilo la usajili litawazuwia watu binafsi pamoja na mataifa, kusafirisha na kufisha fedha kwa kupitia makampuni ya biashara ya majumba. Na hawatoweza tena kuficha utajiri wao kwa ununuziwa majumba mjini humo.
Mji wa London umekuwa kivutio kikubwa cha biashara ya kimataifa ya majumba, na serikali inakisia kwamba makampuni ya kigeni yanamiliki zaidi ya majumba 100,000 nchini kote, na nusu yake zikiwa mjini London.
Hata hivyo Cameron binafsi alishutumiwa vikali hivi karibuni kuhusiana na ukwepaji wa kulipa kodi, pale jina lake lilipoorodheshwa katika nyaraka za siri za Panama.
Nyaraka zilodhihirisha majina ya viongozi na watu mashuhuri mbalimbali duniani, wanaomiliki fedha na mali nje ya nchi zao kwa lengo la kukwepa kulipa kodi. Kiongozi huyo alipinga shutuma hizo kwa kuweka wazi takwimu za mapato yake na kodi alizotozwa.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman