1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kiuchumi kati ya Marekani na Afrika mjini Dakar

Mohammed AbdulRahman18 Julai 2005

Naibu waziri wa Marekani asema rushwa bado ni kikwazo kwa vitenga uchumi na biashara

https://p.dw.com/p/CHfq

Mataifa ya kiafrika yameanza kuamka na kupambana na tatizo la rushwa, lakini pamoja na hayo rushwa bado ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya biashara na vitega uchumi kati ya Marekani na bara hilo. Hayo yameelezwa na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika Thomas Woods wakati ukifanyika mkutano wa kiuchumi baina ya Marekani na Afrika ulioanza Jumatatu katika mji mkuu wa Senegal-Dakar.

Naibu huyo waziri wa Marekani alisema kwamba kwamba nchi yake ina wasi wasi na sera na taratibu zinazokwamisha kuwepo kwa mazingira bora kwa biashara na utendaji.

Katika mahojiano sambamba na mutano wa kiuchumi kati ya Marekani na Afrika katika mji mkuu wa Senegal-Dakar, Bw Woods alisema baadhi ya nchi za kiafrika zimepiga hatua ya maendeleo katika kupambana na rushwa, kwa kuunda tume na kuwatia nguvuni watuhumiwa, ambao ni kutoka tabaka za chini. Lakini akaongeza kwamba hayo hayatoshi kupambana kikamilifu na tatizo hilo, bali hadi pale wanapokamatwa vigogo wahusika na rushwa na kushitakiwa. Bw Woods ambaye ni naibu waziri wa mambo ya nchi za nje anayehusika na masuala ya Afrika, alisema hilo litakua suala kuu katika mkutano huo wa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi utakaoendelea hadi Jumatano .

Wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka mataifa 37 ya kiafrika watajadiliana juu biashara, vitenga uchumi na masuala ya utawala wa kiraia, pamoja na ujumbe wa Marekani unaoongozwa na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Bibi Condoleeza Rice, wakiwemo wawakilishi wa makampuni makubwa ya Kimarekani yanayotafuta biashara na kandarasi . Mbali na mawaziri wanashiriki pia waakilishi kutoka sekta ya biashara ya binafsi na jumuiya za kiraia.

Jukwaa hilo linatokana na ule mpango wa Marekani wa miaka mitano chini ya kile kinachoitwa sheria inayohusiana na ukuaji na nafasi za kiuchumi kwa kimombo Growth and Opportunity Act- AGOA kwa ufupi, ambayo imeondoa ushuru wa forodha na kodi ya uagizaji bidhaa kutoka n´gambo kwa kiasi ya bidhaa 6,400 mbali mbali, kuanzia maadini hadi matunda kama embe na kadhalika, zinazoingia Marekani kutoka nje.

Naibu waziri Woods amepongeza mafanikio ya utaratibu huo, ambao amesema umeinua bidhaa zinazosafirishwa nje na mataifa ya kiafrika kusini mwa jangwa la Sahara zinazoingizwa Marekani, kwa 88 asili mia kutoka kipindi cha matumizi ya fedha cha 2003 hadi 2004, na kufikia hadi kiasi ya dola 26 bilioni.

Kadhalika bidhaa zinazosafirishwa na Marekani katika eneo hilo ziliongezeka kwa 25 asili mia hadi dola bilioni 8.6 mwaka jana, ongezeko la maradufu ikilinganishwa na sehemu nyengine za dunia. Vitenga uchumi vya moja kwa moja vya Marekani vilifikia dola bilioni 11.5 hadi mwisho wa mwaka 2003.

Lakini Bw Woods anasema waafrika vangali wakikabiliwa na changa moto katika kuendeleza zaidi biashara na kuvutia vitega uchumi, na hasa sekta ya uchumi kama mafuta, maadini na bidhaa nyengine za kuvutia.

Alisema Afrika inahitaji kuimarisha nyenzo zinazoinua biashara ambazo ni pamoja na miundo mbinu ya uhakika, masoko, kupambana na vizzi vinavysababishwa na ushuru pamoja na kuimarisha harakati na mikakati ya kusaka masoko nchi za nje.

Aidha naibu huyo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika alisema, rushwa na hongo, ni visa vinavyoivunja moyo Marekani panapohusika na uwekezaji katika nchi za Kiafrika, na vitendo hivyo vinahujumu uwezo na maendeleo ya biashara katika nchi hizo zenyewe.

Alizitaja nchi kama Zambia na Afrika kusini kuwa mfano mzuri katika jitihada za kuipiga vita rushwa. Itakumbukwa Makamu wa rais Jacob Zuma alifukuzwa kazi mwezi Juni mwaka huu baada ya kuhusishwa katika mkasa wa rushwa katika kesi dhidi ya mshauri wake mmoja wa zamani wa masuala ya biashara. Alisema nchi hizo zimeonyesha dhamira ya thati kupambana na tatizo hilo-lakini akaongeza kwamba bado kuna mengi yanayopaswa kufanywa.

Wakati huo huo, Bw Woods aligusia juu ya matumaini ya kuiona Ivory coast ikirejea haraka kuwa miongoni mwa nchi za kiafrika zinazonufaika na mpango wa Marekani wa nafuu za kibiashara , baada ya kuondolewa mapema mnwaka huu, kutokana na kupamba moto kwa mgogoro kati ya serikalii na waasi katika nchi hiyo -mlimaji mkubwa wa kokoa duniani.

Akazipongeza juhudi zinazoongozwa na Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini kuleta amani nchini Ivory coast akisema, Marekani itafuatilia kwa makini matokeo ya uchaguzi utakaofanyika Ivory coast baadae mwaka huu, kama njia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini katika taifa hilo la Afrika magharibi.