Mkutano wa kitaifa waanza Madagascar
13 Septemba 2010Mkutano wa kitaifa wa wiki moja kuutatua mzozo wa kisiasa nchini Madagascar umefunguliwa hii leo asubuhi nje ya mji mkuu Antananarivo huku wawakilishi wa viongozi wakuu wa kisiasa wakiususia mkutano huo.
Mjadala huo unaotarajiwa kudumu muda wa wiki nzima untarajiwa kugusia masuala ya serikali ya mpito,katiba mpya,maandalizi ya uchaguzi unaokuja pamoja na uwiano wa kitaifa.
Takriban wanachama 4000 wa mashirika ya kijamii na wanasiasa wa vyama mbali mbali wanaotoka miji yote nchini humo walikuwepo katika mkutano huo unaofanyika nje ya mji mkuu wa Antananarivo.
Washirikishi wa viongozi wakuu wa kisiasa,akiwemo rais aliyepinduliwa Marc Ravalomanana,aliyemtangulia Didier Ratsiraka na Albert Zafy, wameususia mkutano huo wakisema kuwa hawataki kuidhinisha jitihada hizi ambazo wanaona hazitafaulu. Habari zinasema hata kiongozi wa sasa Andry Rajoelina hakushiriki.
Viongozi hao watatu wa zamani wanasisitiza juu ya kuandaliwa mazingira muwafaka ya kurejea kutoka uhamishoni kwa Ravalomanana na Ratsiraka pamoja na kuvunjwa kwa serikali ya sasa ya mpito. Tangu alipoangushwa na Rajoelina kwa msaada wa wanajeshi, Ravalomanana anaishi Afrika kusini na Ratsiraka anaishi uhamishoni nchini Ufaransa.
Tarehe 13 mwezi uliopita wa Agosti, vyama kiasi ya 150 vya kisiasa kisiwani Madaagascar wakiwemo wanasiasa wanaojitegemea binafsi na waliokaribu na Bw Ravalomanana, vilisaini mkataba wa kisiasa vikiwa na shabaha ya kujaribu kufungua ukurasa mpya wa maelewano, ili kuutatua mgogoro huo wa kisiasa. Mkataba huo ukatoa wito wa kuitishwa mkutano wa kitaifa, kuzungumzia mustakbali wa kisiasa wa taifa hilo.
Madagascar Imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu mwishoni mwa 2008 na hali ikazidi kuwa mbaya baada ya kuangushwa Ravalomanana tarehe 17 Machi 2009,mapinduzi ambayo hayakutambuliwa na jamii ya kimataifa.
Bado inasubiriwa kura ya maoni mwezi Novemba kama ilivyosisitizwa katika makubaliano yaliofikiwa, na kura hiyo kufuatiwa na uchaguzi wa bunge Machi mwaka ujao na ule wa rais mwezi wa Mei.
Hata hivyo bado kuna utata juu ya ratiba hiyo,kutokana na vikwazo vinavyomkabili rais wa zamani Ravalomanana, baada ya kuhukumiwa hivi karibuni, kwa makosa ya ubadhirifu wa mali ya umma na mauaji yaliofanywa na walinzi wake, wakati wa maandamano ya wapinzani, yaliokuwa chanzo cha vuguvugu la kumuondoa madarakani.Wapi inaelekea Madagasacar ni suala litakaloweza kujibiwa zaidi na matokeo ya mkutano huo wa kitaifa .
Mwandishi:Maryam Abdulla/AFP
Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman