Mkutano wa kimataifa wa usalama waanza Munich
1 Februari 2013Mkutano wa usalama wa mjini Munich ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1963, katikati ya vita baridi. Ulianzishwa kama mkutano wa mataifa wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO ukiwa na lengo la kuzungumzia mgogoro kati ya mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani na yale ya Mashariki yakiongozwa na iliyokuwa Jamhuri ya Kisoviet.
Baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin mwaka 1989, mkutano wa Munich ulianza pia kuzungumzia matatizo katika nchi za Ulaya ya Kati na Magharibi. Ilifuata pia mijadala kuhusu hali kwenye nchi za Kiasia. Hivi sasa mkutano huo ni kielelezo cha utandawazi na sera za kimataifa za masuala ya usalama.
Washiriki wa kimataifa
Miongoni mwa nchi 70 zinazohudhuria mkutano wa mwaka huu unaofanyika kuanzia tarehe 1 Februari hadi tarehe 3 Februari yapo mataifa yanayoibukia kiuchumi kama vile India, China na Brazil. Mataifa ya Kiafrika nayo yamewakilishwa. Kati ya washiriki wapatao 400 hawapo wanasiasa tu, bali pia viongozi wa nyanja za kiuchumi pamoja na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
"Kongamano la kimataifa la Munich juu ya usalama linaonyesha mabadiliko kwenye utungaji wa sera za usalama katika karne ya 21," anaeleza Wolfgang Ischinger, mwenyekiti wa mkutano huo. "Mbali na mada kali kama sera za usalama tunazungumzia pia mada nyepesi zaidi kama vile mabadiliko ya tabia ya nchi au usalama katika mtandao wa internet."
Kiongozi mashuhuri zaidi katika mkutano wa mwaka huu ni makamu wa rais wa Marekani Joe Biden. Mwaka 2009 Biden alishiriki pia katika mkutano huo, ambapo alizungumzia uhusiano wa nchi yake kwa Urusi. Waziri wa mambo ya nje wa Brazil pamoja na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya uhalifu ya ICC, Fatou Bensouda, watashiriki kwa mara ya kwanza.
Kubadilishana mawazo bila woga
Mkutano wa Munich unajikita zaidi katika mijadala kuhusu vita, namna ya kuzuia migogoro na mipango ya kupunguza akiba za silaha. "Kongamano hili linatoa nafasi ya kipekee kuzungumzia vitisho vya usalama wa kimataifa na wawakilishi wa nchi zote muhimu, mashirika ya kimataifa na yale yasiyo ya kiserikali," anaeleza Professor James Davis wa chuo kikuu cha St. Gallen. Yeye ameshiriki katika mkutano huo kwa miaka kumi iliyopita.
Faida nyingine anayoiona Davis ni kwamba hakuna maamuzi yanayopitishwa Munich. Mkutano unawapa tu nafasi washiriki kupanuo ufahamu na kupata mawazo mapya juu ya sera za usalama. Kwa kuwa mkutano haupitishi maamuzi rasmi, na rahisi zaidi kwa viongozi kuzungumza wazi zaidi kuhusu mada zinazojadiliwa.
Mwandishi: Michael Knigge
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Khelef