1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kimataifa wa usalama umeanza leo mjini London Uingereza.

28 Januari 2010

Unalenga kujadili hali ya usalama nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/LikT
Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown (kulia), na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan (kushoto),wakipiga picha kabla ya kuanza kwa mkutano wa kimataifa wa usalama mjini katika ukumbi wa Lancaster mjini London hii leo.Picha: AP

Mkutano wa Kimataifa juu ya usalama nchini Afghanistan umeanza leo mjini London, Uingereza, huku Rais Hamid Karzai wa nchi hiyo akisema kabla kwamba ana imani serikali ya nchi yake itachukua udhibiti wa usalama katika majimbo yote 34 ifikapo mwaka 2015.

Lakini akasema anatarajia vikosi vya kigeni vitaendelea kuwepo nchini humo kwa muongo mmoja. Mkutano huo umefunguliwa kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown kusema kwamba mazungumzo hayo ya mjini London yanaashiria mwanzo wa mchakato wa makabidhiano ya udhibiti wa usalama kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kwenda kwa Afghanistan.

"Huu ni wakati muhimu sana kwa jumuiya ya kimataifa ambayo imekuwa ikiwasaidiwa watu wa Afghanistan kuweza kujitawala.

Na mkutano huu ni mwanzo wa mpango wa mpito wa kuwakabidhi majukumu ya kiusalama kutoka kwa majeshi ya kimataifa kwenda kwa vikosi vya Afghanistan na wananchi wenyewe" .Alisema Waziri Mkuu Brown.

Mazungumzo hayo ya mjini London yanakuja katikati ya mashaka makubwa juu ya hali ya Afghanistan, ikiwa ni zaidi ya miaka minane sasa nchi hiyo ikipigana na wapiganaji wa Taliban, mapigano yaliyosababisha vifo kwa maelfu ya watu na kuuvuruga kabisa mustakabali wa nchi hiyo.

Nchi zilizo nyuma ya mpango huo wa Afghanistan zinaangalia namna ya kuijenga upya nchi hiyo pamoja na kuongeza misaada ya maendeleo, lakini zinatarajiwa kumpa mbinyo zaidi Rais Karzai kupambana na rushwa ambayo imekwamisha juhuid za kutekelza mageuzi muhimu.

Katibu Mkuu wa Nato; Anders Fogh Rasmussen; ametoa onyo hii leo kwa viongozi wanaohudhuria mkutano huo kwamba juhudi na kujitolea kwa vikosi vya kigeni hazitoshi kumaliza matatizo ya Afghanistan, bali kunatakiwa mpango madhubuti wa kuboresha utawala unaozingatia maslahi ya raia.

Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje 20 wameuonya mkutano huo wa kimataifa wa usalama kwamba bila hatua za haraka za kuuboresha uchumi wa Yemen unaodidimia, vita dhidi ya ugaidi vitazidi kuwa vigumu, kwani eneo hilo linaelekea kuwa makazi mapya ya kudumu ya Al-Qaeda.

Onyo hilo la pamoja limekuja kufuatia mazungumzo ya saa mbili ya mawaziri hao mjini London, na kuongeza kwamba matatizo ya Yemen yatalizorotesha Bara Arabu kama hayatatafutiwa ufumbuzi wa mapema.

Mwandishi:Lazaro Matalange/APE/AFP

Mhariri: Miraji Othman