Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya wafanyika Brussels
16 Desemba 2021Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels leo kwa mkutano wa kilele unaojikita kwa sehemu kubwa kujadili ushirikiano na mataifa ya Ulaya mashariki pamoja na kitisho cha aina mpya ya kirusi cha corona, Omicron, barani Ulaya.
Suala la kusambaa kwa kirusi cha Omicron ndiyo litakuwa ajenda ya juu kwenye mkutano wa leo mjini Brussels huku viongozi wa kanda hiyo watajaribu kutafuta mkakati wa pamoja wa kudhibiti kusambaa kwake.
Tathmini iliyotolewa hivi karibuni kwamba kirusi hicho ndiyo kitakuwa chanzo cha maambukizi mengi ya Covid-19 kwenye mataifa ya Ulaya ifikapo mwezi Januari mwaka unaokuja imezusha hamkani na wasiwasi mkubwa wa kutokea mzozo wa kiafya.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya hawataki mparaganyiko mipakani
Viongozi wanaokutana mjini Brussels wanataka kukomesha migawanyiko ndani ya kanda hiyo hasa kuhusu kanuni za usafiri baada ya Italia na Ugiriki kujiunga na Ureno kutangaza masharti ya nyongeza kwa wasafiri kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakijadili kwa wiki kadhaa njia madhubuti ya kuratibu sera ya safari wakilenga kuzuia kusambaa kwa kirusi cha Omicron bila kuzusha mshike mshike kwenye mipaka ya kanda ya Schengen ambayo watu husafiri bila vikwazo.
Hata hivyo siku ya Jumanne Italia ilitangaza kwamba kuanzia tarehe 16 Disemba itawataka wasafiri wote kutoka mataifa ya Ulaya kuonesha uthibitisho wa kutokuwa na maambukizi ya Covid-19 hata kama wamepatiwa chanjo kikamilifu. Ikiwa hilo litatekelezwa, kuna wasiwasi wa kutokea mparaganyiko wa shughuli za uchukuzi kwenye kanda ya Ulaya na viongozi wengi wanataka hilo liepukwe.
Urusi, Belarus na mfumuko wa bei pia vitajadiliwa
Suala lingine litakayoumiza vichwa vya wakuu wa nchi wa Umoja wa Ulaya ni pamoja na mvutano wake na Urusi kutokana na Moscow kupeleka maelfu ya wanajeshi wake karibu na mipaka ya Ukraine.
Akizungumzia suala hilo wakati akiwasili kwenye ukumbi wa mikutano kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema "Tutajadili hali ngumu nchini Ukraine, suala la kurundikwa wanajeshi kwenye mpaka. Na kwa hivyo leo tutasisitiza tena kwamba kuheshimu sheria za mipaka ni moja ya misingi muhimu sana ya amani barani Ulaya na kwa pamoja tutafanya kila linalowezeka ili hilo la kuheshimu sheria za mipakani liendelee"
Mbali ya msuguano na Urusi, viongozi wa Umoja wa Ulaya watatupia jicho pia suala la mzozo wa wakimbizi unaotikisa mipaka ya kanda hiyo hasa kati ya Poland, iliyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya na Belarus inayotuhumiwa kuwakaribisha maelfu ya wakimbizi kutumia ardhi yake kuingia Ulaya.
Kadhalika kadhia ya kupanda kwa bei za nishati kulikochochea mfumuko wa bei ndani ya kanda ya Ulaya itakuwa sehemu ya kile viongozi wa Umoja wa Ulaya watajaribu kutafuta majibu hivi leo mjini Brussels.