1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa shirika la FAO mjini Roma

Oumilkher Hamidou17 Novemba 2009

Hakuna ratiba maalum iliyopangwa kuifyeka njaa ulimwenguni

https://p.dw.com/p/KYvs
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la FAO Jacques DioufPicha: AP

Viongozi wa taifa na serikali waliokusanyika jana mjini Roma nchini Italy,wameahidi "kufyeka balaa la njaa linalowasumbua watu bilioni moja ulimwenguni."Hawakupanga lakini Ratiba.

Hali hiyo imemkera sana mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la chakula na kilimo-FAO Jacques Diouf."Iliwahi kuzungumziwa juu ya mwaka 2025,lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa na hali hii imenisikitisha sana" amesema mkurugenzi mkuu wa FAO,Jacques Diouf wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari mjini Roma."Sikuridhika kwasababu hakuna tarehe iliyopangwa,kiwango cha fedha wala masharti kwa ahadi za misaada zilizotolewa" amesisitiza akiongeza hata hivyo kusema ameridhika na ile hali kwamba "maridhiano yamepatikana kuhusu taarifa ya mwisho."

Katika hati hiyo iliyoidhinishwa mara baada ya mkutano kuanza,viongozi wametilia mkazo umuhimu wa kufikiwa lengo la Millenium la kupunguza kwa nusu idadi ya watu wanaosumbuliwa kwa njaa na ukosefu wa chakula bora hadi ifikapo mwaka 2015.

Dhamiri hizo lakini zilitajwa pia mwezi June mwaka jana.Na tangu wakati huo idadi ya wanaosumbuliwa na njaa imeongezeka kutoka watu 850 milioni na kufikia bilioni moja nukta sifuri mbili.

Vitega uchumi vinavyohitajika kuinua shughuli za kilimo havikutajwa pia.Mkurugenzi mkuu wa FAO Jacques anaashiria patahitajika jumla ya dala bilioni 120,dala bilioni 44 kati ya hizo kama msaada wa kimataifa na dala bilioni 76 kutoka nchi husika.

Tangu mwanzo wa mkutano huo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon alizungumzia hesabu zinazotisha aliposema watoto 17 elfu wanakabiliwa na kitisho cha kufa kwa njaa kwa siku-watoto milioni sita kwa mwaka.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amehimiza pawepo mageuzi ya kina kuweza kupata chakula,kuwalinda masikini kupita wote na wasiojiweza.Anasema ili kuweza kuwalisha zaidi ya watu bilioni tisaa mnamo mwaka 2050,mazao ya kilimo yatabidi yaongezeke kwa asili mia 70.

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Benedikt wa 16 amekosoa "hali ya kujipendelea" na ulanguzi katika soko la nafaka.Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni amesema:

Papst Benedikt vor Abflug nach Afrika
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Benedikt wa 16.Picha: AP

"Tatizo la usalama wa chakula lazma lifumbuliwe kwa kuzingatia matumaini ya kudumukuondowa chanzo cha matatizo na kuinua shughuli za kilimo katika nchi maskini."

Viongozi wasiopungua sitini kutoka mataifa ya Afrika,Asia na Latin Amerika wamejibu mwaliko wa shirika la umoja wa mataifa la Chakula na Kilimo-FAO kuhudhuria mkutano huo mjini Roma.

Kwa upande wa mataifa tajiri kiviwanda G-8,pekee Italy ndio iliyowakilishwa na waziri mkuu Silvio Berlusconi.

Mashirika kadhaa yasiyomilikiwa na serikali yameyakosoa makampuni makubwa makubwa ya vyakula,kutaka kudhibiti mamilioni ya hekari za ardhi zenye rutuba kutoka wakulima wadogo wadogo wa nchi za ulimwengu wa tatu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (AFP)

Mhariri: Abdul-Rahman