1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa nishati ya Diesel Magazetini

Oumilkheir Hamidou
2 Agosti 2017

Mkutano wa viongozi wanaohusika na sekta ya usafiri, jinsi jumuia ya kimataifa inavyoikodolea macho China na jinsi kampeni za uchaguzi mkuu zilivyopamba moto nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini .

https://p.dw.com/p/2hYEj
Symbolbild Dieselskandal
Picha: picture-alliance/dpa/J. Stratenschulte

Tunaanzia Berlin ambako wajerumani wanasubiri kwa hamu matokeo ya mkutano muhimu wa viongozi wote wanaohusika na sekta ya usafiri humu nchini . Mkutano huo unaitishwa kufuatia kashfa zinazozidi kufichuliwa kuhusiana na magari yanayotumia nishati ya Diesel. Gazeti la "Westfalenpost" linaandika: "Hata kabla ya mkutano huo wa kilele uliopewa jina "Mkutano wa kilele wa Diesel" kuanza, matokeo yake tayari yanajulikana. Si ajabu kuona kwamba katika mkutano muhimu kama huo, taarifa za mwisho zinaenezwa, na katika kadhia hii kuchapishwa mapema taarifa zinazoutaja mkutano huo kati ya wanaviwanda na wanasiasa kuwa si chochote chengine isipokuwa kiini macho. Kwamba wanasiasa wa ngazi ya juu mfano wa waziri mkuu wa  jimbo la North Rhine Westphalia Armin Laschet wanatoa masharti makubwa makubwa hata kabla ya mkutano kuanza, ni hadaa tu. Au wanafikiri wananchi ni majuha?"

China yaimarisha nguvu za kijeshi

Gazeti la "Frankenpost" " linazungumzia jinsi walimwengu wanavyoiangalia jamhuri ya umma wa China kwa hisia za mchanganyiko. Gazeti linaendelea kuandika: "Walimwengu wanaliangalia dola hilo kuu katika eneo la mashariki ya mbali kwa  jicho la mchanganyiko wa hisia za kuvutia lakini pia kwa jicho la wasi wasi. China inamezewa mate kwa jinsi ilivyogeuka haraka mno kuwa dola la viwanda. Hofu na wasi wasi unatokana na pale rais wa China alipozungumzia hadharani kuhusu kuundwa "jeshi la aina pekee ulimwenguni." Xi Jinping amesema kinaga ubaga jeshi hilo linabidi liwe na uwezo wa kupigana vita. Katika ikulu ya Marekani  kauli mbiu ya rais Trump "Marekani kwanza" ndio inayofuatwa na matokeo yake yatakua kuidhoofisha jumuia ya kujihami ya magharibi. Viongozi wa mjini Beijing wanaiangalia hali hiyo kuwa ni sawa na kibali cha kujipanua."

SPD na kampeni ya uchaguzi mkuu

 

Kampeni za uchaguzi mkuu zimepamba moto nchini Ujerumani. Katika wakati ambapo utafiti wa maoni ya wananchi unaashiria vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU vinaongoza, chama cha Social Democratic SPD kinafafanua malengo yake. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika: "Mbinu za Martin Schulz kutaka kuwaambia wapiga kura wachague kati ya Angela Merkel na yeye zinaonyesha hazimsaidii kitu. Na kwa vyovyote vile: hali ya kiuchumi na kijamii si mbaya kuwafanya wapiga kura wapiganie mageuzi katika uongozi wa serikali. Licha ya matatizo yote yaliyoko. Wananchi wanahisi mambo ni mazuri pamoja na Angela Merkel na hata kama si mazuri, mwengine pia hatoweza kuyafanya yawe bora.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga