1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa NATO waishupalia China

Daniel Gakuba
14 Juni 2021

Viongozi wa nchi za jumuiya ya kujihami ya NATO wanafanya mkutano wa kilele mjini Brussels, wakichukua msimamo mkali dhidi ya China, kwa hoja kwamba mienendo ya Beijing ni changamoto kwa mfumo wa utangamano wa kidunia.

https://p.dw.com/p/3utR9
Belgien Brüssel | Joe Biden im Gespräch mit Jens Stoltenberg
Picha: Stephanie Lecocq/AP/picture alliance

Katika tangazo la pamoja la viongozi hao kabla ya kuanza mkutano wao, wameelezea wasiwasi unaosababishwa na sera za China, ambazo jumuiya ya NATO inasema ni za kichokozi, na zinakwenda kinyume na maadili ya jumuiya hiyo ya kujihami. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi 30 wanachama wa umoja huo wa kijeshi kuafiki matumizi ya lugha kali dhidi ya China ambayo kila kukicha inazidi kuimarika kiuchumi.

Soma zaidi:  Biden aanza ziara yake ya kwanza ya kigeni

Mkutano wao wa mwisho mwaka 2019 uliishia kutambua kuwa kutanuka kwa ushawishi wa China kuna faida inayoambatana na changamoto kwa NATO.

Biden asema Urusi na China zina mienendo ambayo haikutarajiwa

Rais wa Marekani Joe Biden ambaye anahudhuria mkutano huo, akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari pamoja na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, ameikosoa tabia ya Urusi na China.

Belgien Brüssel | Joe Biden im Gespräch mit Jens Stoltenberg
Joe Biden ambaye anahudhuria mkutano wa kilele wa NATO kwa mara ya kwanza kama rais wa MarekaniPicha: Stephanie Lecocq/AP/picture alliance

''Tumetambua katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kwamba tunakabiliwa na changamoto mpya, inayotokana na Urusi ambayo imekuwa na mienendo ambayo hatukuitarajia, na mienendo ambayo hata China inaikumbatia,'' amesema Biden.

Soma zaidi: Biden, Stoltenberg waujadili mkutano ujao wa NATO

Kuangaziwa zaidi kwa China kunatokana na hisia za Joe Biden ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza kama rais wa Marekani, lakini wanachama wengine, husasan nchi za Ukanda wa Baltiki zinazopakana na Urusi, bado zinaichukulia Moscow kama kitisho kikubwa zaidi kwa usalama wao.

NATO yajipanga kuelekea siku za usoni

Hofu kubwa ya jumuiya ya NATO kuhusu China inasabibishwa na kuongezeka kwa uwezo wa nchi hiyo katika sekta ya silaha za nyuklia, na ushirikiano wa karibu na Urusi ambao umehusisha luteka za kijeshi za pamoja.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amemuarifu Rais Biden kuwa jumuiya hiyo imejiandaa kwa kuweka mkakati madhubuti kwa siku za usoni.

Brüssel NATO Gipfeltreffen | Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwasili katika mkutano wa NATO mjini BrusselsPicha: Brendan Smialowski/AFP/AP/picture alliance

Amesema, ''Tunajenga ruwaza kabambe ya 2030 kuhusu mustakabali wa NATO, ambao unatutaka zuwekeze zaidi katika muda wa miaka saba ijayo, na hicho ndicho tunachokifanya. Tumeongeza bajeti ya ulinzi kwa dola bilioni 260 za ziada kutoka nchi za Ulaya na Canada.''

Soma zaidi: China yaliponda kundi la G7 kwa 'upotoshaji'

Lakini pia mkutano huu unaacha mlango wazi kwa ushirikiano baina ya NATO na China, katika masuala kama kupambana na mabadiliko ya tabia.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema hakuna kiongozi yoyote wa nchi mwanachama wa NATO anayenuia kuanzisha vita baridi vipya kati yao na China.

Kushiriki kwa Rais Biden kumeleta ahueni katika Jumuiya ya NATO, baada ya misukosuko iliyosababishwa na utawala wa miaka minne wa mtangulizi wake Donald Trump.

 

Vyanzo: rtre, dpae