1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya SADC kufanyika Jumatatu Namibia

Josephat Nyiro Charo14 Agosti 2010

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anatarajiwa kuuambia mkutano huo wa siku mbili, kwamba Zimbabwe imepiga hatua katika uendeshaji wa shughuli za serikali ya umoja wa kitaifa

https://p.dw.com/p/OndB
Rais wa Afrika Kusini, Jacob ZumaPicha: AP

Viongozi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, watakutana Jumatatu ijayo mjini Windhoek Namibia kujadiliana kuhusu serikali ya Umoja wa kitaifa ya Zimbabwe ambayo imekabiliwa na matatizo makubwa na hatua ya serikali hiyo kukataa kuyazingatia maamuzi yaliyopitishwa na jopo la jumuiya hiyo.

Mkutano ya mjini Windhoek kirasmi unaadhimisha miaka 30 tangu kuasisiwa kwa jumuiya ya SADC. Wakati huo nchi za jumuiya hiyo zilijukana kama nchi zilizokuwa msitari wa mbele kuratibu harakati za ukombozi nchini Namibia na Afrika Kusini iliyokabiliwa na ubaguzi wa rangi. Tangu Namibia ilipojipatia uhuru wake na kumalizika kwa utawala wa Wazungu nchini Afrika Kusini, jumuiya hiyo imekuwa ikisuasua kujidhihirisha kama chombo cha kisiasa, kwa sababu wanachama wake hawako tayari kutekeleza maamuzi yanayopitishwa na kanda hiyo.

Mada kuu itakayougubika mkutano huo wa SADC, ni hali nchini Zimbabwe, ambayo ilisaini mkataba wa kuundwa kwa mahakama ya kanda hiyo mjini Windhoek, lakini ikakataa kutii hukumu zilizotolewa na mahakama hiyo.

Präsident Robert Mugabe Simbabwe
Rais wa Zimbabwe, Robert MugabePicha: AP

Mahakama ya jumuiya ya SADC imepitisha hukumu kuwapendelea wakulima Wazungu nchini Zimbabwe, ikisema mageuzi ya sheria kuhusu ardhi, yaliyofanywa na rais wa nchi hiyo Robert Mugabe, yaliwalenga Wazungu kwa maonevu kutokana na uasili wao. Serikali ya mjini Harare imekataa katakata uamuzi huo wa kuwaruhusu wakulima hao warejee kwenye mashamba yao, hivyo kuzusha maswali kuhusu lengo la kuwa na mahakama maalumu ambayo haiwezi kutekeleza maamuzi yake.

Katibu mtendaji wa jumuiya ya SADC, Tomaz Salomao, amesema mawaziri wa sheria wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo watawasilisha ripoti kuhusu ukaidi wa Zimbabwe. Afrika Kusini nayo pia itawataarifu viongozi kuhusu maendeleo yaliyopatikana kwenye serikali ya Umoja wa kitaifa. Wizara ya mambo ya kigeni ya Afrika Kusini imesema rais wa nchi hiyo Jacob Zuma ameelezea matumaini yake kuhusu serikali ya mseto ya Zimbabwe, akisema inaendesha shughuli zake kwa njia inayofaa.

Simbabwe Krisengipfel SADC
Katibu mtendaji wa jumuiya ya SADC, Tomaz Augusto SalomaoPicha: AP

Mkurugenzi mtendaji wa wizara hiyo, Ayanda Ntsaluba, amesema rais Zuma atauambia mkutano wa SADC mjini Windhoek kwamba kazi nchini Zimbabwe haijakamilika, lakini picha jumla ni ya kutia moyo. Zuma atawaambia viongozi wa jumuiya hiyo kwamba kuna ishara ya uthabiti nchini Zimbabwe na mambo yanaelekea kuwa shwari.

Rais Zuma ndiye mpatanishi rasmi wa jumuiya ya SADC katika mzozo wa Zimbabwe na aliitembelea nchi hiyo mnamo mwezi Machi mwaka huu, kumshinikiza rais Mugabe na waziri mkuu Morgan Tsvangirai kusuluhisha tofauti zao kuhusu uteuzi wa nyadhifa muhimu serikalini na kusukuma mbele mchakato wa mageuzi nchini humo. Hakuna ufanisi wowote uliopatikana kufikia sasa katika juhudi za kuutanzua mzozo juu ya hatua ya rais Mugabe kumteua gavana wa benki kuu na mwanasheria mkuu.

Kwa mujibu wa mkataba wa kugawana madaraka, Zimbabwe ilitakiwa kufanya kura ya maoni kuhusu katiba mpya mwezi uliopita, ambayo ingefungua mlango wa kufanyika uchaguzi mpya kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2008 uliozusha utata.

Viongozi wote wa nchi wanachama wa jumuiya ya SADC wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa mwaka mjini Windhoek, isipokuwa Madagascar, ambayo uanachama wake bado umesitishwa kufuatia mapinduzi ya mwaka jana yaliyofanywa na meya wa zamani wa jiji la Antananarivo, Andrey Rajoelina, akisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.

Viongozi hao watajadiliana juu ya mipango ya kuinganisha jumuiya ya SADC na Soko la pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, COMESA na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baadhi ya nchi wanachama wa SADC ni wanachama wa COMESA au jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kukwamisha juhudi za kuwa na umoja wa forodha na kuainisha sheria za kibiashara.

Hatimaye kanda hizo tatu zinasema zitaungana na kuunda eneo huru la kibiashara la Afrika litakalokuwa na wanachama 26 kuanzia Cape Town Afrika Kusini hadi Cairo Misri.

Mkutano wa SADC nchini Namibia unatarajiwa kumalizika siku ya Jumanne wiki ijayo.

Mwandishi: Charo, Josephat/ AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman