Mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Tunis
31 Machi 2019Viongozi wa mataifa matatu ya kiarabu, Algeria, Sudan na Moroko wameamua kutoshiriki katika mkutano huo wa kilele wa siku moja unaotarajiwa kupinga uamuzi wa Rais Trump na kuutaja kuwa "batili". Hayo ni kwa mujibu wa rasimu ya taarifa ya mwisho ya mkutano huo wa kilele." Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa Golan ni ardhi ya Syria inayokaliwa-" amesema hayo mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Ahmed Abu Gheith mjini Tunis.
"Tangazo lolote na la kutoka nchi yoyote linalokana ukweli huo ni batili kisheria " ameongeza kusema.
Uamuzi wa rais Trump kuhusu Golan ni batil
Uamuzi wa Rais Trump kuhusu milima ya Golan unafuatia uamuzi kama huo alioupitisha mwaka jana alipotangaza kuhamishia Jerusalem kutoka Tel Aviv ubalozi wa Marekani nchini Israel na kuzusha hasira katika ulimwengu wa kiislam.
Rais Bashar al Assad wa Syria hakualikwa kuhudhuria mkutano huo wa kilele . Nchi yake imesitishiwa uanachama kufuatia matumizi ya nguvu yaliyomwaga damu dhidi ya vuguvugu la kudai mageuzi ya kidemokrasi mwaka 2011.
Mbali na Golan, mzozo wa Israel na Palastina na vita vya Yemen ni miongoni mwa mada mkutanoni
Lakini mnamo miaka ya hivi karibuni baadhi ya mataifa ya kiarabu yameanza kuijongelea serikali ya Bashar al Assad.
Msemaji wa jumuia ya nchi za kiarabu Mahmoud Afifi amesema kwa upande wake viongozi wamedhamiria kuonyesha mshikamano na kutoa taarifa inayotilia mkazo msimamo wa kimataifa kuwa milima ya Golan ni ardhi ya Syria inayokaliwa na Israel. Mbali na suala hilo viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu watazungumzia uwezekano wa kuitambua upya Syria kama manachama, watajadili kuhusu mzozo wa Israel na Palastina na pia uhasama kati ya Saudi Arabia na Iran na vita nchini Yemen.
Mandisshi:Hamidou Oummilkheir/AP/dpa
Mhariri: Daniel Gakuba