Mkutano wa kilele wa jumuia ya NATO mjini Lisbon
19 Novemba 2010Viongozi wa jumuia ya kujihami ya NATO wanakutana kuanzia leo mjini Lisbon nchini Ureno kwa mkutano wa siku mbili,wakitarajiwa kuamua kuhusu kurejeshwa nyumbani wanajeshi wao kutoka Afghanistan hadi ifikapo mwaka 2014 na kutegwa mtambo wa kinga dhidi ya makombora barani Ulaya.
Marekani na washirika wake 27 wanataka kuanza kuikabidhi Afghanistan opereshini zote za kijeshi,hatua baada ya hatua kuanzia robo ya kwanza ya mwaka ujao."Kipindi hicho cha mpito" kitakamilika mwishoni mwa mwaka 2014.
Mada nyengine kuu katika mkutano huo wa kilele wa mjini Lisbon zinahusu mfumo wa kinga dhidi ya makombora barani Ulaya,kuifanyia marekebisho jumuia ya kujihami ya NATO na kuanzisha ushirikiano pamoja na Urusi.
Hii leo viongozi wa taifa na serikali wa jumuia ya kujihami ya NATO wataanza mkutano wao kwa kujadili "mkakati mpya" utakaoiongoza jumuia yao katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Mbali na somo gumu lililopatikana nchini Afghanistan,viongozi wanataka kupanga mbinu za namna ya kukabiliana na vitisho vya aina mpya:ambavyo ni pamoja na ugaidi,vita vya mtandao,uharamia na kitisho cha kutapakaa silaha za kinuklea duniani.
Washirika 28 wanatazamiwa pia kuamua kuhusu mpango wa kumiliki mtambo wa kinga dhidi ya makombora ili kuihami Ulaya.
Wataamua pia taasisi za NATO zipunguzwe.
Kesho jumamosi mazungumzo yatatuwama kuhusu Afghanistan,kwa kuitishwa mkutano wa mataifa 48 yanayochangia wanajeshi wa kimataifa wanaolinda amani nchini humo na kuongozwa na jumuia ya NATO-ISAF,akihudhuria pia rais Hamid Karzai na waziri mkuu wa Japan.
Baadae viongozi wa NATO watakutana na rais Dmitri Medvedev kwa mkutano wa kilele kati ya NATO na Urusi-mkutano unaotazamiwa kuimarisha ushirikiano baada ya mvutano uliosababishwa na vita kati ya Urusi na Georgia mnamo mwaka 2008.
Akizungumzia kuhusu uhusiano kati ya nchi yake na jumuia ya NATO,rais Dmitri Medvedev amesema:
"Uhusiano kati ya NATO na Urusi umeanza kuwa wa maana na wa nguvu tangu miezi vya hivi karibuni.Kwa namna hiyo imefunguka njia ya kuweza kubuni mfumo wa ulinzi barani Ulaya na ulimwenguni kwa jumla."
Inategemewa pia kuiona Urusi ikiruhusu treni zinazosafirisha vifaa vya NATO zipite katika nchi za Balkan kuelekea Afghanistan.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters
Mpitiaji:Yusuf Saumu