1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kilele wa G20 kuimarisha uchumi duniani

15 Novemba 2014

Mkutano wa Kundi la G20 wa nchi zenye nguvu kubwa za kiuchumi na zile zinazoinukia kiuchumi umefunguliwa nchini Australia Jumamosi (15.11.2014) ajenda ikiwa kuimarisha ukuaji wa kiuchumi duniani.

https://p.dw.com/p/1Do3u
Mkutano wa Kilele wa Kundi la G20 mataifa yenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani mjini Brisbane Australia. (15.11.2014)
Mkutano wa Kilele wa Kundi la G20 mataifa yenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani mjini Brisbane Australia. (15.11.2014)Picha: Reuters

Barack Obama wa Marekani, Vladimir Putin wa Urusi,Angela Merkel wa Ujerumani,Dilma Roussef wa Brazil,Narendra Modi wa India na Jacob Zuma wa Afrika Kusini ni miongoni mwa viongozi wanaouhudhuria Mkutano huo wa Kilele wa siku mbili unaofanyika katika mji wa Brisbane.

Akifunguwa rasmi mkutano huo wa Tisa wa Kilele wa G20 Mwenyekiti wa kundi hilo la G20 na Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott amesema ujumbe ambao unapaswa kutoka kwao katika siku mbili za mkutano huo ni ujumbe wa matumaini na kwamba viongozi hao watawasilisha mpango wa kuongezea dola trilioni mbili kwa pato la jumla duniani na kuahidi biashara huru na uwekezaji zaidi katika miundo mbinu.

Amesema mipango hiyo ya kukuza uchumi itaongeza ajira kwa mamilioni na kuongeza pato la jumla duniani kwa zaidi ya asilimia mbili ikiwa ni juu ya kiwango kilichokuwa kikitegemewa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Ujumbe kwa dunia

Abott amekaririwa akisema "Ndio, tunataka biashara huru na tutaiwasilisha.Ndio tunahitaji miundo mbinu zaidi na tutaijenga."

Rasi Barack Obama wa Marekani akiwa na Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbot katika Mkutano wa Kilele wa G20 mjini Brisbane. (15.11.2014)
Rasi Barack Obama wa Marekani akiwa na Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbot katika Mkutano wa Kilele wa G20 mjini Brisbane. (15.11.2014)Picha: Reuters

Ameongeza kusema huo ni ujumbe wao kwa dunia: kwamba serikali zinaweza kuwasilisha, kwamba serikali zinaweza kukubaliana kwamba dunia inaweza kuwa bora, kunaweza kuwepo kazi za juu, ukuaji mkubwa wa kiuchumi na ajira zaidi.

Mataifa ya kundi la G20 ambayo yanawakilisha asilimia 85 ya uchumi wa dunia yako chini ya shinikizo kuchukuwa hatua madhubuti katika mkutano huu wa kilele badala tu ya kutoa mkururo wa malengo yenye kubabaisha yasiokuwa na vipimo.

Merkel : Hali ya Ukraine haikubaliki

Mzozo wa Ukraine umeutia kiwingu mkutano huo ambapo kauli za wanasiasa wengi zimehodhiwa na suala hilo kwa kuilani Urusi kwa madai kwamba inausaidia uasi mashariki mwa nchi hiyo.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema Umoja wa Ulaya unafikiria vikwazo zaidi vya kifedha dhidi ya watu binafsi wa Urusi kutokana na mzozo huo wa Ukraine.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika Mkutano wa Kilele wa G20 mjini Brisbane. (15.11.2014)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika Mkutano wa Kilele wa G20 mjini Brisbane. (15.11.2014)Picha: picture-alliance/RIA Novosti/S. Guneev

Merkel amewaambia waandishi wa habari kwamba hali ilioko sasa hairidhishi na kwamba kwa sasa suala la kuwaorodhesha watu wengine kwenye vikwazo hivyo liko kwenye ajenda.

Merkel ambaye alikuwa akitarajiwa kukutana na Rais Vladimir Putin pembezoni mwa mkutano huo wa kilele amesema hatarajii kuwepo kwa mabadiliko ya ghafla na ya maana kufuatia mkutano wake huo.

Urusi yashutumiwa

Akizungumza pembezoni mwa mkutano huo, Rais Barack Obama wa Marekani ameishutumu Urusi kwa kufanya uchokozi wa kutisha dhidi ya Ukraine na kusema jambo hilo ni tishio kwa dunia.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy ambaye pia anahudhuria mkutano huo ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba Urusi lazima ikomeshe upelekaji wa silaha na vikosi nchini Ukraine na kwamba lazima iviondowe vikosi vyake ambavyo tayari viko nchini humo. Ameongeza kusema kwamba Urusi inaweza ikawekewa vikwazo zaidi na Umoja wa Ulaya.

Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na Mwana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Salman bin Albdulaziz Al Saud. mjini Brisbane. (15.11.2014)
Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na Mwana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Salman bin Albdulaziz Al Saud. (15.11.2014)Picha: Getty Images/R. Griffith

Urusi mara kwa mara imekuwa ikikanusha kuhusika kwa njia yoyote ile katika mzozo wa Ukraine ambapo umegharimu maisha ya zaidi ya watu 4,000 tokea kuanza kwake hapo mwezi wa Aprili.

Ebola na mazingira katika mjadala

Viongozi hao baadae walitoa taarifa juu ya janga la Ebola huko Afrika magharibi kwa kuzihimiza nchi ambazo hazikuchangia katika juhudi za kupambana na ugonjwa huo kufanya hivyo hivi sasa na kutuma timu za matibabu.

Mazungumzo hayo ya Brisbane mbali na uchumi pia yanagusia mazingira ambapo Obama ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kabla ya mkutano huo wa kilele kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Waandamanaji wakipinga Mkutano wa Kilele wa G20 mjini Brisbane.(15.11.2014)
Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na Mwana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Salman bin Albdulaziz Al Saud. mjini Brisbane. (15.11.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Obama ameahidi kutoa dola bilioni 3 kusaidia kugharamia juhudi za athari za mabadiliko ya tabia nchi katika nchi za kimaskini.

Australia juu ya kwamba ni mojawapo ya nchi zilizoathirika sana na kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani imekuwa ikisita kuliweka suala hilo kwenye ajenda ya mkutano huo baada ya kufuta kodi ya utowaji wa hewa ukaa.

Mkutano huo unamalizika hapo Jumapili kwa utoaji wa taarifa rasmi kuelezea kile nchi ilichoweza kufanikisha na inachotaka kufanikisha katika kipindi cha usoni.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/Ap/dpa AFP

Mhariri :Caro Robi