1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kimataifa wakutana Roma

Nijimbere, Gregoire3 Juni 2008

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon, ameufungua mkutano wa kilele wa shirika la kilimo na chakula FAO mjini Roma Italy akitoa mwito wa kufanya juhudi za kuongeza uzarishaji wa kilimo

https://p.dw.com/p/EBsL
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-MoonPicha: AP

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa mkutano huo wa siku tatu mbele ya viongozi wa nchi na serikali wapatao 50, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon, amesema mataifa duniani hayana budi kuzipitia sera za kilimo zilizokuwepo na kuzifanyia marekebisho fulani ili kuongeza uzarishaji wa kilimo kwa lengo la kupambana na hali ya mfumko wa bei za vyakula ambao tayari imejitokeza. Sera katika sekta hiyo ya kilimo, zapaswa kuhakikisha kwamba watu watapa chakula sio tu mnamo siku za usoni bali pia kwa muda mrefu. Ban Ki-Moon amesema:

" Kunahitajika kuongezeka uzarishaji wa kilimo kwa asili mia 50 ifikapo 2030 ili kutimiza mahitajio ya chakula ambayo yamezidi kupanda. Hii ni fursa ya kihistoria ya kuimarisha sekta ya kilimo".


Ban Ki-moon amezidi kusema kuwa litakuwa jambo la busara kama sera zitakazotumika zitaepusha kuziporomosha nchi nyingine.

Kwa hiyo ni bora nchi zihakikishe kwamba sekta ya kilimo imepata gharama za kutosha na wala sio mikopo.


Mbali na hayo, Ban Ki-Moon ametoa mwito wa haraka wa kuidhinisha mkataba wa shirika la biashara duniani WTO wa mjini Doha ambao umekuwa na raundi nyingine ya mazungumzo na ambao unapendekeza kuondolewa kwa sera juu ya biashara na ushuru ambazo zimeharibu masoko.

Mkutano huo wa mjini Roma uliitishwa kufuatia taarifa za tahadhari zilizotolewa na Benki kuu ya dunia kwamba watu kiasi ya bilioni mbili sasa wanakabiliwa na ongezeko kubwa la bei duniani na miongoni hao takriban milioni 100 wanakabiliwa na hatari ya kuanguka katika hali ya umasikini kutokana na kuzidi kupanda kwa bei za chakula.

Kwa hakika bei hizo za chakula zilipanda mara mbili kwa muda wa miaka mitatu tu katika nchi kadhaa na kusababisha maandamano na uharibifu wa mali na vitu katika nchi kama vile Misri na Haiti.

Mfumko huo wa bei ulipelekea pia baadhi ya nchi za kiafrika, Brazil, India, Vietnam na Misri kuchukuwa hatua za kubana chakula kilichokuwa kikiuzwa katika nchi za nje.

Kupanda kwa bei ya mafuta, sera mbaya za kibiashara, mahitajio ya chakula kuzidi kuongezeka, mavuno madogo na kupanda kwa bei ya uchukuzi, vyote hivyo vimezungumziwa kama sababu za mfumko wa bei za chakula unaoshuhudiwa mnamo siku hizi.


Mkutano huo wa mjini Roma Italy juu ya chakula, umeshuhudia pia lawama dhidi ya marais wawili ambao ni miongoni mwa wanaoshiriki. Hao ni pamoja na rais wa Iran Mahamoud Ahmadinejad na rais wa Zimbabwe Robert Mugabe. Rais wa Iran amepingwa hasa na Israeli kupitia balozi wake mjini Roma kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya Israeli huku rais Robert Mugabe akipingwa hasa na Uingereza na Australia kufuatia hali mbaya ya haki za binaadamu nchini kwake.