Mkutano wa jumuiya ya NATO waingia siku ya pili mjini Bucharest
3 Aprili 2008Mkutano wa jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi, NATO, umeingia siku yake ya pili hii leo mjini Bucharest nchini Romania. Kikao cha leo kinajadili kwa kina upanuzi wa jumuiya hiyo na Afghanistan.
Viongozi wa NATO wanaanza mazungumzo kwa kina kuhusu Afghanistan hii leo baada ya siku ya kwanza ya mkutano wa mjini Bucharest kuonyesha ufanisi mkubwa kwa Ufaransa kuahidi kuepeleka wanajeshi zaidi nchini Afghanistan. Msemaji wa NATO amethibitisha kwamba rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameahidi kutoa kikosi cha wanajeshi kati ya 700 hadi 800 kwenda katika eneo linalokabiliwa na machafuko kusini mwa Afghanistan kuondoa kitisho cha Canada kutaka kuwaondoa wanajeshi wake kutoka eneo hilo.
Ajenda ya mkutano wa Bucharest unamleta rais wa Afghanistan, Hamid Karzai na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kwa mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa NATO na wajumbe kutoka nchi zilichochangia wanajeshi katika kikosi cha kimataifa nchini Afghanistan kinachoongozwa na jumuiya hiyo.
Rais Karzai ameishukuru jumjuiya ya NATO kwa kazi yake ya miaka kadhaa nchini Afghanistan lakini akasisitiza wanahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa na wanajeshi zaidi ili kuvishinda vita dhidi ya ugaidi na kujenga taasisi zitakazosimamia usalama nchini humo.
Rais George W Bush wa Marekani amesema jumuiya ya NATO ina jukumu la kuisadia Afghanistan.
"Vita nchini Afghanistan haviwezi kushindwa kwa nguvu zetu pekee. Lazima pia tuisaidie serikali ya Afghanistan kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kutoa huduma muhimu, kutengeneza nafasi za ajira na kuwaonyesha Waafghanistan kuwa uhuru wao unaweza kuwaletea maisha mazuri. Lakini kwa hili kufanyika Afghanistan inahitaji usalama, na NATO ianajaribu kusaidia."
Mapema leo viongozi 26 wa jumuiya ya NATO wameanza kufanya kikao cha kwanza rasmi cha mazungumzo kujadili mada zilizojitokeza jana wakati wa chakula cha jioni, zikiwemo upanuzi wa NATO, Kosovo, Afghanistan na maswala mengine. Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema leo ufanisi utaonekana kuhusu Afghanistan na swala la upanuzi wa NATO.
Hali ya kutoelewana kuhusu upanuzi wa jumuiya ya NATO imejitokeza kwenye mkutano wa Bucharest. Vita vya maneno kati ya rais George W Bush wa Marekani na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kuhusu hatima ya maombi ya Ukraine na Georgia kutaka kujiunga na jumuiya ya NATO. Rais Bush anataka nchi hizo ziruhusiwe kujiunga na NATO pamoja na mataifa mengine ya Balkan.
"Tutaamua ikiwa tukubali maombi ya mataifa mengine mawili ya Balkan, Bosnia Herzegovina na Montenegro, zianze mazungumzo na NATO. Marekani inaziunga mkono nchi hizi na tutaweka wazi kuwa mlango pia uko wazi kwa Serbia."
Lakini kansela Merkel kwa upande wake anasema bado ni mapema mno.
"Nigependa kwamba Macedonia, Albania na Croatia zote kwa pamoja zikubaliwe kujiunga na NATO. Tutafanya kila juhudi hadi dakika za mwisho za mkutano huu kuusuluhisha mgogoro uliopo. Lakini bado sina hakika ikiwa tutafaulu hivi leo."
Msemaji wa jumuiya ya NATO, James Appathurai, ameashiria kwamba Albania na Croatia zitaalikwa kujiunga na jumuiya hiyo kwenye mkutano wa Bucharest. Viongozi wa nchi hizo leo wataonja utamu wa baraza kuu la NATO watakapofanya kikao maalum na katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Jaap de Hoop Scheffer pamoja na viongozi wengine.
Tatizo lengine lililojitokeza katika kikao cha jana ni hatua ya Ugiriki kukataa kubadili msimao wake kuhusu kitisho cha kutumia kura yake ya turufu kuzuia uanachama wa Macedonia mpaka nchi hiyo ibadili jina lake kutambua wasiwasi wa serikali ya mjini Athens kuhusu eneo la kaskazini mwa Ugiriki linaloitwa pia Macedonia.