Mkutano wa hali ya hewa waanza Copenhagen.
8 Desemba 2009Karibu wajumbe 15,000 kutoka nchi 192 wamekusanyika katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen, kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa. Katika hotuba yake ya ufunguzi, mwendeshaji mkuu wa majadiliano katika mkutano huo, wa Umoja wa Mataifa, Yvo de Boer alisema mkutano huo utaweka historia lakini lazima iwe historia inayofaa.
Wapatanishi wengi hawana matumaini ya kupatikana kwa mkataba utakaouchukua nafasi ya mkataba wa Kyoto, lakini Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon ameelezea matumaini yake kwamba makubaliano mapya yanaweza kuafikiwa. Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amezitolea wito nchi nyingi kupunguza zaidi viwango vyao vya gesi zinazoharibu mazingira, akisema China na India lazima zifanye jitihada za ziada. Merkel atakuwa miongoni mwa viongozi 103 watakaohudhuria mkutano huo wa siku 12.