Mkutano wa hali ya hewa mjini Copenhagen
7 Desemba 2009Mkutano mkubwa kabisa wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa unaowaleta pamoja wajumbe 15 elfu kutoka mataifa 192 umefunguliwa mjini Copenhagen.
Lengu lake kuu ni kubuni mkataba wa aina mpya,au angalao kufungua njia ya kufikiwa mkataba mpya utakaochukua nafasi ya itifaki ya Kyoto ambayo awamu ya kwanza inamalizika mwaka 2012-ili kuepukana na balaa la kuzidi hali ya ujoto inayosababishwa na moshi unaotoka viwandani.Madhara ya hali hiyo hayana kifani.
Wakuu kadhaa na mashirika wametoa taarifa za kutia moyo ,mfano katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon,Shirika la mazingira la Umoja wa mataifa na waziri mkuu wa Danemark Lars Lokke Rasmussen ambae nchi yake ndio mwenyeji wa mkutano huu wa wiki mbili.
"Ulimwengu unatega matumaini yake kwenu nyie katika kipindi hiki kifupi cha historia ya ubinaadam" amesema waziri mkuu wa Danemark,Rasmussen alipokua akifungua mkutano huo .Ameongeza kusema tunanukuu"Makubaliano hayako mbali kufikiwa."Mwisho wa kumnukuu.
Waziri wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani Norbert Röttgen amejiwekea shabaha maalum anasema:
"Tunahitaji maamuzi thabiti.Jumuia ya kimataifa inabidi iahidi hali ya ujoto haitoachiwa kuongezeka kwa zaidi ya centigrad mbili za Celcius. Hilo tuu ndilo litakalodhamini misingi ya maisha yetu."
Viongozi 110 wa taifa na serikali kutoka kila pembe ya dunia watahudhuria mkutano wa kilele,katika awamu ya mwisho ya mkutano huu utakaomalizika December 18 ijayo.
Kuhudhuria viongozi wote hao "ni ushahidi wa mwamko usiokua na kifani katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.Ni fursa ambayo ulimwengu haustahiki kuiachia ipite vivi hivi" amesema waziri mkuu wa Danemark.
Viongozi wa taifa na serikali hawakushiriki katika mkutano uliopita wa mawaziri wa mazingira mnamo mwaka 1997 mjini Kyoto nchini Japan.
"Jukumu la mwisho linawaangukia raia wa dunia ambao ndio watakaoathirika na madhara ya kushindwa kufikiwa makubaliano."Amesisitiza waziri mkuu wa Danemark Lars Lokke Rasmussen.
Mtihani mkubwa katika mkutano huu uliolengwa kukamailisha juhudi za miaka miwili za mazungumzo yaliyoanzia Bali December mwaka 2007,ni kuondoa hali ya kutoaminiana na mivutano kati ya ulimwengu tajiri wa viwanda na ulimwengu uliosalia,tangu maskini mpaka ule wa nchi zinazojiendeleza kiviwanda.
Nchi tajiri zinakabiliana na kundi la nchi 77 zinazoinukia.Mivutano inahusu kiwango cha fedha zilizolengwa kuzisaidia nchi maskini kuweza kujiambatanisha na mabadiliko ya hali ya hewa na kuanza kufuata utaratibu wa kiuchumi usiochafua sana mazingira ,pamoja na kukubaliana juu ya njia za kupunguza viwango vya moshi unaotoka viwandani.
Ili kushinikiza makubaliano yaweze kufikiwa,magazeti 56 kutoka nchi 45 yamechapisha uhariri wa pamoja kuzitaka nchi zote,maskini na tajiri zioneshe mshikamano mjini Copenhagen.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Reuters,AFP)
Mhariri:Abdul-Rahman